Waziri Mkuu wa Afrika Kusini Auawa kwa Kuchomwa Visu Bungeni!

 

MWANDISHI: WALUSANGA NDAKI| RISASI JUMAMOSI| NAKUJUZA ZAIDI

KWA wanaokumbuka, siku hiyo shule zilifungwa, wafanyakazi serikalini waliowahi kazini asubuhi walirudi nyumbani baada ya kuambiwa siku hiyo ilikuwa sikukuu.

Kwa kifupi, siku hiyo – Septemba 6, 1966 — ilikuwa ni siku ya furaha kwa Watanzania.

Ni miaka zaidi ya 50 iliyopita siku Watanzania na wapenda uhuru na amani duniani walifurahi bila kificho baada ya kupata habari za kufa kwa aliyekuwa waziri mkuu wa Afrika Kusini, Hendrik Frensch Verwoerd, aliyechomwa visu na Mzungu mwenzake aliyeitwa Dimitri Tsafendas.

Kaburu Verwoerd (hutamkwa Fevuat) ndiye mwasisi mkuu wa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa watu wa Afrika Kusini, kufuatana na rangi zao,

akatenga maeneo watu waishi kufuatana na rangi zao!

Hivyo, Weupe, Weusi, Machotara na Waasia wakaishi sehemu zao na Wazungu (Weupe), waliokuwa hawafikii hata milioni mbili wakawatawala watu wa rangi zingine waliokuwa zaidi ya milioni 30 wakati huo!

Weupe wakaamua kila kitu chini ya ubaguzi huo wa rangi uliolaaniwa duniani ukijulikana kwa neno la Kikaburu la ‘apartheid’ ambao ulianzishwa na Kaburu huyo mwaka 1948 hadi ulipoangamia mwaka 1994 mbele ya walimwengu.

Verwoerd ndiye aliyekipandisha chama kikuu cha Makaburu cha National Party (South Africa), hadi akawa waziri mkuu tangu Septemba 2, 1958 alipoongeza ukatili hususan dhidi ya weusi kupitia polisi, mashushushu na jeshi la ulinzi.

Waliopinga ubaguzi walikamatwa, wakazuiliwa majumbani mwao, wakatupwa magerezani, wakalazimika kuikimbia nchi hiyo, wakateswa au kuuawa ambapo Verwoerd akaifanya nchi hiyo kuwa Jamhuri ya Afrika Kusini mwaka 1961. Alivipiga marufuku vyama vya kupinga ubaguzi vya African National Congress (ANC) na Pan Africanist Congress (PAC) na kuanzisha Mashitaka ya Rivonia yaliyowatupa gerezani Mandela na wenzake.

Mzungu mmoja aliyeuchukia ubaguzi, David Pratt, alijaribu kumuua Verwoerd Aprili 9, 1960, eneo la Milner Park, jijini Johannesburg.

Pratt aliyekuwa mkulima na mfanyabiashara, alimfyatulia Verwoerd risasi mbili kutoka kwenye bastola, moja ikalichana vibaya shavu la kulia na kulifumua sikio lake la kulia pia kabla ya walinzi na maofisa kumnyang’anya bastola.

Verwowerd alianguka akivuja damu, akakimbizwa Hospitali ya Johannesburg ambapo baada ya siku mbili madaktari walisema hali yake ilikuwa ya kuridhisha na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Pretoria. Madaktari walisema alipona kifo kimaajabu na walipomwondolea risasi walijua asingeweza tena kusikia na kutembea bila kuyumba.

Hata hivyo, Mei 29 baada ya miezi isiyozidi miwili, alirejea kazini akiwa mzima. Pratt alikiri alikuwa amedhamiria kumuua mwasisi huyo wa ubaguzi wa rangi. Hata hivyo, alionekana na matatizo ya akili, hakushitakiwa, akapelekwa hospitali ya magonjwa ya akili ambako Oktoba 1, 1961, siku ya 53 ya kuzaliwa kwake, alijinyonga.

Hata hivyo, miaka sita baadaye akiwa bado waziri mkuu, Verwoerd aliuawa jijini Cape Town wakati anaingia Bungeni mchana saa 8:15 ambapo Dimitri Tsafendas alimchoma visu mara nne shingoni na kifuani kabla ya kukamatwa na wabunge na kukimbizwa hospitali alipofia njiani.

Kama ilivyokuwa kwa Pratt, Tsafendas naye alikwepa adhabu ya kifo kutokana na kuwa na matatizo ya akili.

Zulia lililokuwa na madoa makubwa ya damu ya Verwoerd baada ya kuuawa, liliendelea kuwemo bungeni humo tangu wakati huo hadi lilipoondolewa mwaka 2004.

Mazishi ya Verwoerd yalihudhuriwa na watu wapatao 250,000 wengi wao wakiwa Wazungu, akamwacha mjane aliyefariki mwaka 2000 akiwa na umri wa miaka 98.


Loading...

Toa comment