The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu wa Japan Anusurika Kifo Kufuatia Mlipuko Mkubwa wa Bomu

0

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amenusurika kifo baada ya kutokea mlipuko uliofuatiwa na moshi mzito alipokuwa akitoa hotuba katika Mkoa wa Wakayama huko Magharibi mwa Japan, tukio lililotokea leo Jumamosi, April 15, 2023.

Taarifa kutoka Shirika la Habari la Japan, NHK zinaeleza kuwa waziri mkuu huyo hajapata madhara yoyote na walinzi wake walifanikiwa kumuondoa eneo la tukio akiwa salama na tayari mtu mmoja amekamatwa katika eneo la tukio.

Vyombo kadhaa vya habari, ikiwa ni pamoja na Shirika la Habari la Kyodo, vimeripoti kwamba kitu kinachofanana na bomu la moshi kilirushwa, lakini ilionekana kuwa hakuna majeraha au uharibifu ulioripotiwa katika eneo la tukio.

Picha za televisheni zinaonesha umati wa watu ukihangaika kisha mlio wa mlipuko ukifuatiwa na utoaji wa moshi mweupe.

Mtu mmoja amekamatwa katika eneo la tukio katika Bandari ya Wavuvi ya Saikazaki katika Mkoa wa Wakayama.

Kishida alikuwa atoe hotuba ya uchaguzi, kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha umma cha NHK ambacho kilirusha picha zinazomuonesha mtu akiwa chini akiwa amezungukwa na watu wengine kadhaa huku umati wa watu ukitawanyika.

Imeelezwa kuwa, mtu huyo amekamatwa kwa tuhuma za kuzuia biashara, kulingana na kituo hicho.

Hakuna uthibitisho rasmi uliotolewa mara moja na mamlaka ya Polisi imekataa kutoa maoni.

Wakati tukio hilo linatokea, muda mfupi Kishida alikuwa amemaliza kuonja samaki na alikuwa anahutubia umati wa watu kumuunga mkono mgombea kutoka chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP) katika uchaguzi mdogo ujao wa ubunge.
Japan imeimarisha mipango yake ya usalama baada ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani, Shinzo Abe, ambaye alipigwa risasi na kuuawa alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kampeni za uchaguzi mwezi Julai, mwaka jana.

Leave A Reply