The House of Favourite Newspapers

Waziri Mtoro, Akamatwa, Awekwa Sandukuni Kurudishwa Nigeria

0

umaru-dikkoNI kituko kilichotokea miaka ipatayo 32 iliyopita! Ni mwaka 1984 ambapo serikali mpya ya Nigeria chini ya Muhammadu Buhari ilitaka  aliyekuwa waziri wa usafirishaji, Umaru Dikko aliyekimbilia nchi za nje, arejeshwe kwa kuiibia Nigeria dola bilioni sita za Marekani, kutokana na mauzo ya petroli.

Mpango wa kumkamata Dikko aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu nchini humo, ‘ilisukwa’ na serikali ya Nigeria na shirika la ujasusi la Israel liitwalo Mossad.  Dikko aliyekuwa waziri wa usafirishaji chini ya utawala wa Shehu Shagari, aliikimbia nchi hiyo na asijulikane alikokuwa baada ya Buhari kutwaa madaraka na kutaka wote ‘waliokwiba’ mali za umma warejeshwe kuadhibiwa.

Hivyo, baada ya kumtafuta kwa muda,  Juni 30, 1984, Mossad ilimgundua akiwa eneo la Queensway,  jijini London, Uingereza, ikaujulisha ubalozi wa Nigeria nchini humo ili wamkamate, kwani jasusi wa Israel aliyemwona, alimfuata kinyemela na kufahamu alikuwa anakaa eneo la Porchester Terrace.

Kabla ya kumkamata, alitayarishwa daktari wa dawa za usingizi ili amchome sindano Dikko ambaye angebebwa ndani ya sanduku la mizigo ya kibalozi au kidiplomasia (diplomatic bag)!
Siku iliyofuata, Julai 4, 1984,  Dikko alitekwa karibu na nyumbani kwake, akadungwa sindano ya usingizi na Dk. Shapiro wa Israel.
Tatizo lilikuwa ni kwamba sekretari wa Dikko aitwaye Elizabeth Hayes, aliona kitendo hicho cha kumteka na  akaripoti polisi haraka.

Ikishiriki mpango huo, serikali ya Nigeria, Julai 3, 1984, ikapeleka ndege London, ili kumchukua Dikko ambaye angefichwa katika sanduku au kasha kubwa, kwa kisingizio kwamba ulikuwa mzigo wa kidiplomasia.

Ndani ya sanduku alimowekwa Dikko, kulikuwa pia na Dk. Shapiro wa kuhakikisha anaendelea kumdunga sindano za usingizi asije akakurupuka na kuvuruga mpango huo hasa uwanjani Stanstead.  Sanduku la pili lilikuwa limewaficha majasusi wa Israel, Alexander Barak na Felix Abithol ambao nao walikuwa wanakwenda Nigeria kukamilisha mpango huo.
Siri hiyo huenda ilikuwa inafahamika kwa maofisa usalama wa Nigeria waliokuja na ‘dege’ kubwa tupu la Nigeria Airways Boeing 707, maalum kubeba ‘mzigo’ huo.

Hata hivyo, tatizo jingine likawa ni kukosekana kwa hati kutoka serikali ya Uingereza za kuruhusu ‘mzigo’ huo wa kibalozi usikaguliwe uwanjani hapo.  Isitoshe, masanduku hayo hayakuwa na ‘lebo’ ya kidiplomasia kama inavyotakiwa kimataifa.

Hivyo, maofisa wa forodha walilazimika kuyafungua masanduku hayo na kukuta watu ndani yake na hivyo kumwokoa Dikko ambaye alipelekwa hospitali na mpango huo ukawa umekufa!
Watu 17 walikamatwa kuhusiana na njama hizo na kuhukumiwa vifungo gerezani nchini Uingereza na kwa kulipiza, Nigeria iliwakamata wahandisi wawili wa Uingereza na kuwatupa gerezani.
Dikko aliyezaliwa Desemba 31, 1936, alikufa Julai 14, 2014 jijini London akiwa na umri wa miaka 77.

Leave A Reply