The House of Favourite Newspapers

Waziri Mwakyembe Atembelea Global, Afunguka Kufungiwa Chaneli

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas (kushoto) akimpokea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe alipofika katika ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori jijini Dar es Salaam leo.

 

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe leo ametembelea Kampuni ya Global Group ambayo ndani yake kuna makampuni mbalimbali ikiwemo ya Global Publishers inayochapisha magazeti.

 

Magazeti yanayochapishwa na kampuni hiyo ni magazeti pendwa ya Uwazi, Ijumaa, Risasi, Amani, Ijumaa Wikienda na yale bora ya michezo nchini ya Championi na Spoti Extra.

 

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally, akisalimiana na Dkt. Mwakyembe baada ya kuwasili ofisi za Global Group.  Wa tatu kutoka kulia ni Meneja Mkuu wa Global Publishers,  Abdallah Mrisho, na kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisso.

Akizungumza na wafanyakazi wa Global Dk. Mwakyembe alisema wizara yake ina mpango wa kuunda chombo ambacho kitasimamia wanahabari na kitaundwa na wana habari wenyewe.

Alisema nia ya kufanya hivyo ni kuboresha tasnia hiyo na pia ana mpango wa kuhakikisha wana habari wanafanya kazi zao kwa weledi na ikiwezekana kuwe na tuzo maalum itakayosimamiwa na kutolewa na chombo hicho.

Dkt. Harrison Mwakyembe akisaini kitabu cha wageni.

Akizungumzia michezo, waziri alisema Serikali inataka kuhakikisha kabla ya mwaka ujao, Tanzania tunakuwa na viwanja bora vya mpira wa miguu vitatu.

“Viwanja hivyo vitakuwa na sehemu maalumu kwa ajili ya wana habari, lakini hayo tutafanya tukipata fedha na tayari Serikali imepitisha bajeti ya jambo hilo,” alisema Waziri Mwakyembe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza akisani kitabu cha wageni.

Akizungumzia sakata la vishumbusi, waziri alisema DSTV, Azam na Zuku walifanya makosa kwa kuvunja sheria makusudi kwa kutoza watu chaneli ambazo hazikupaswa kutozwa fedha.

“Tutakuwa taifa la ajabu kama tutaruhusu taarifa za habari kutozwa tozo, kwamba ili mtu aone taarifa ya habari basi ni lazima alipie, kama Serikali hatuwezi kuruhusu hilo,” alisema Waziri Mwakyembe.

Saleh Ally akimwonyesha Mwakyembe magazeti yanayotolewa na Global Publishers.

Alisema wote wanaotaka kuonesha habari za ndani wanapaswa kulipia leseni ya kufanya hivyo lakini wale waliokatazwa hawakuwa na leseni na mitambo yao ya kurushia matangazo yao ipo nje ya nchi.

“Wakitaka kurusha mambo ya ndani ya nchi yetu wanaweza kung’oa mitambo yao iliyo nje ya nchi na waje kuisimika hapa kwetu, Kisarawe, Kibaha na kadhalika wakiwa na leseni ya kufanya hivyo,” alisisitiza waziri.

Aliipongeza Kampuni ya Global Group kwa kufanya kazi kwa weledi na kwa jinsi alivyoona, wafanyakazi wanafanya kazi kwa ari kwa kuona kuwa ni yao, huku akisisitiza kuwa amevutiwa na kila kitu alichokiona katika ziara yake hiyo.

Katika ziara hiyo alikuwepo pia Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Dk. Hassan Abbas, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mungereza na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisso.

Dkt. Mwakyembe akiongea na wafanyakazi wa Global Group akiwa na Dkt. Hassan Abbas  na Meneja wa Global Group, Abdallah Mrisho (kulia).

Viongozi hao walitembezwa katika ofisi mbalimbali za Global Group na Mhariri Mtendaji, Saleh Ally aliyekuwa ameambatana na Meneja Mkuu, Abdallah Mrisho kabla ya kufanya kikao alichoruhusu maswali kutoka kwa wafanyakazi hao.

Wafanyakazi wa Global Group wakimsiliza Dkt. Mwakembe.
Dkt. Mwakyembe akijibu maswali ya wafanyakazi.
…Taswira ilivyokuwa wakati wa mkutano.
Waziri Mwakyembe akiwa na baadhi ya wafanyakazi wa Global Group.

PICHA NA MUSA MATEJA | GPL

Comments are closed.