The House of Favourite Newspapers

Waziri Mwijage: Nani kasema sukari ya ndani haitoshi?

0

DSC_0409Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ,Charles John Mwijage.

Elvan Stambuli na Sifael Paul

Charles John Mwijage ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Awamu ya Tano aliyeteuliwa katika Baraza la Mawaziri la mwanzo la Rais John Pombe Magufuli. Ni mbunge wa kuchaguliwa kutoka Jimbo la Muleba Kaskazini mkoani Kagera kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika mahojiano maalum ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Mwijage ameliambia Uwazi kuwa serikali imelivalia njuga suala la uagizaji wa sukari kutoka nje ikiwa na lengo la kuja na suluhisho kwa kutengeneza kwanza mfumo sahihi wa uagizaji wa sukari. Pia amegusia mambo mengi yanayoigusa moja kwa moja wizara yake hiyo, ungana nasi;

Baada ya wizara yako kuamuru bei ya sukari isizidi shilingi 1,800 kwa kilo, wafanyabiashara wengi sehemu mbalimbali nchini wamepuuza wito huo, je, nini msimamo wa wizara yako?

Jibu: Ni kweli serikali iliamuru iwe hivyo na kama kuna wafanyabiashara wanafanya hivyo tunalifuatilia na kama tulivyosema serikali haina nia mbaya, lengo ni kutengeneza mfumo wa uagizaji wa sukari kutoka nje. Hicho ndicho kinachofanyika na tumedhamiria kuwa na mfumo sahihi wa uagizaji wa sukari.

Kuna mvutano mkubwa kwamba sukari iliyopo nchini inatosheleza mahitaji lakini baadhi ya wataalam wanasema bidhaa hiyo haitoshi hivyo kitolewe kibali ili sukari ya nje iingizwe, unazungumziaje suala hilo?

DSC_0399

Mwijage (kulia), akifanya mahojiano na waandishi wa habari wa Global Publishers, Elvan Stambuli (wa pili kushoto) na Sifael Paul (wa kwanza kushoto).

Jibu: Sukari inatosha au haitoshi? Naweza kusema inatosha lakini inatosha kwa siku ngapi? Wanaosema haitoshi wanapaniki bila sababu. Serikali itatoa utaratibu wa kuagiza sukari lakini ni lazima kwanza hiyo inayosemekana haitoshi au inatosha tujue ni kwa siku ngapi? Kila kitu kina utaratibu ndiyo maana katika suala hili tumeanza kwa kuweka utaratibu kwanza. Wafanyabiashara hawana sababu ya kupaniki.

Tanzania ya Magufuli ni Tanzania ya viwanda, je, wizara yako ina mpango gani wa kufufua viwanda vilivyokufa nchini?

Jibu: Kwanza tumeanza mkakati mkubwa wa kufufua viwanda ambavyo havifanyi kazi ili vifanye kazi. Swali tuliloanza kujiuliza ni kwa nini viwanda vyetu havifanyi kazi? Tumeamua kufufua viwanda vyetu vifanye kazi, kama kuna wamiliki watakaoshindwa kuviendesha, wawape wengine waviendeshe. Hatutavitaifisha viwanda vilivyoshindwa, tunachotaka vifanye kazi. Malengo ya serikali na wizara kwenye viwanda ni matatu.

Kwanza; Lazima viwanda vyetu vizalishe bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya Watanzania. Siyo kuzalisha tu bali vizalishe bidhaa zenye viwango vya kushindana na bidhaa za nchi nyingine. Hatuna sababu ya kutembea wakati wenzetu wanakimbia.
Pili; Lengo la serikali ni kuona viwanda vinazalisha nafasi nyingi za ajira kwa vijana. Kufufua viwanda vilivyokufa na kuanzisha vipya ni fursa ya kutatua tatizo kubwa la ajira nchini.

La tatu na la mwisho ni kuongeza pato la taifa na kipato cha mtu mmoja mmoja. Ukiwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa kisha watu wakawa na ajira, basi watakuwa na kipato kitakachowawezesha kununua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu na pato la taifa litakua.

Wawekezaji wamehodhi maeneo makubwa ya viwanda bila kujenga viwanda vyenyewe, je, ni hatua gani wanazochukuliwa na serikali?

Jibu: Ni kweli kuna watu walipewa maeneo makubwa ili wajenge viwanda lakini hawayafanyii kazi, msimamo wa serikali ni kwamba walioyatelekeza maeneo ya viwanda lazima wayafanyie kazi kwa kujenga viwanda. Mwaka 1992-1996 serikali iliamua kuwapa watu binafsi au makampuni binafsi viwanda.Tunataka vyote vilivyobinafsishwa vifanye kazi. Tunaelewa kwamba katika soko huria huwezi kumlazimisha mtu azalishe aina fulani ya bidhaa lakini tunachotaka sisi ni viwanda vyetu vizalishe bidhaa zozote watakazozalisha. Hivi sasa tunachambua sababu za baadhi ya viwanda kutofanya vizuri, watakaoshindwa, tutawapa wengine, hatutaifishi.

Serikali iliahidi kwa watu wa mikoa ya kusini kwamba, gesi asilia ikianza kuzalishwa itakwenda sambamba na ujengwaji wa viwanda hasa mkoani Mtwara, je, ahadi hiyo imeanza kutekelezwa?

Jibu: Ujengwaji wa viwanda kusini ya nchi yaani Mtwara ni mkakati wa serikali hii hasa baada ya uzalishaji wa gesi asilia. Ijulikane kwamba sisi kama serikali au wizara hatujengi viwanda, serikali ilishajiondoa katika kufanya biashara badala yake viwanda vinajengwa na sekta binafsi. Kimsingi biashara ikichangamka kwa kuchagizwa na viwanda kutakuwa na maendeleo. Mkakati huo upo, kipo kiwanda tayari cha Msangaa Mkuu, Mtwara kinazalisha mbolea.

Tumeshaweka utaratibu ambapo mwekezaji lazima akubaliane na utaratibu wetu lakini pia anataka ahakikishiwe upatikanaji wa gesi. Mwekezaji wa korosho naye hivyohivyo. Pale Kilwa (mkoani Lindi) pia tayari kuna kiwanda cha mbolea na kiwanda cha mihogo, Mtwara kuna Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mwekezaji huyu alivutiwa na malighafi iliyopo pale.

Leave A Reply