Waziri Ndalichako Alivyozindua Mkutano wa Wastaafu Watarajiwa wa PSSSF
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako, amefungua semina elekezi kwa Wastaafu watarajiwa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) jijini Dar es Salaam Septemba 11, 2023.
Akizungumza na wastaafu hao kutoka mkoa wa Dar es Salaam, alisema Mfuko wa PSSSF umeandaa semina hiyo kwa lengo la kuwajengea wastaafu wake watarajiwa uelewa na ufahamu juu ya umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi ya kukuza vipato vyao baada ya kustaafu ili kuleta tija na uendelevu wa kipato.
“Usia wangu kwenu ni kuyatumia vyema madini ya elimu mtakayoyapata hapa kwa kushikilia mambo makuu matatu nayo ni Kuwa na mtazamo chanya, Kuweka mipango makini na Kutimiza ndoto binafsi baada ya kustaafu.” Alisema Profesa Ndalichako.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema PSSSF inatarajia kuwa na wastaafu 11,000 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
Alisema Wastaafu watapatiwa mafunzo ya elimu ya uwekezaji katika masoko ya fedha, taarifa za nyaraka na utaratibu wa kufuata wakati wa kustaafu, kujiandaa kisakolojia baada ya kutoka kwenye utumishi, umuhimu wa kutunza mazingira tunayoishi kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, na uhalifu wa kimtandao ambao unawaathiri wastaafu wengi.
“Mfuko katika kutambua na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, una mpango wa kutoa mche mmoja wa mti kwa kila mstaafu wa PSSSF, mpaka sasa tuna wanachama 739,000 na lengo hapa ni kila mmoja aweze kupanda na kuutunza mche tutakaompatia.”Alifafanua CPA. Kashimba.
Semina kama hii ilifanyika mwaka 2021 kwa wastaafu watarijiwa 3700 bara na visiwani.