The House of Favourite Newspapers

Waziri Ulega Ashukuru Wakazi wa Mkuranga Kupatiwa Huduma ya Afya ya Macho Bure

Mkazi wa Mkuranga (aliyevaa miwani) akipata huduma ya macho kutoka kwa mtaalamu.

Mkuranga, Pwani – Taasisi ya Bilali Mission Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Yas Tanzania wamefanikisha zoezi la utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure kwa wakazi wa Mkuranga, mkoani Pwani.

Zoezi hilo limewaleta pamoja wananchi wengi waliopata fursa ya kupimwa macho na kupatiwa matibabu bila gharama yeyote.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na baadhi ya waliofika kupata huduma ya macho.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua huduma hizo, Mkurugenzi wa Yas Tanzania, Aidan Komba, alisema:

“Kusogeza huduma za afya ya macho kwa jamii ni sehemu ya dhamira yetu ya kusaidia kuimarisha afya ya Watanzania. Tunafurahi kuona ushirikiano wetu na Bilali Mission Tanzania ukiwanufaisha wananchi wa Mkuranga.”

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga, Mhe. Abdallah H. Ulega, aliwashukuru waandaaji kwa juhudi zao na kuwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi.

“Huduma hizi ni muhimu sana kwa wananchi wetu, nawashukuru Yas Tanzania na Bilali Mission kwa kuhakikisha wananchi wa Mkuranga wanapata matibabu haya muhimu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama hawa ili kuboresha maisha ya wananchi wetu,” alisema Mhe. Ulega.

Zoezi hilo limeonekana kuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Mkuranga, huku likitarajiwa kuimarisha afya ya macho na kuongeza ufanisi wa maisha ya kila siku.