The House of Favourite Newspapers

Waziri wa Elimu: Ratiba ya Kufungua Shule Ipo Vilevile, Akanusha Taarifa za Uzushi

0

 

Serikali imekanusha taarifa za uzushi zilizotolewa kuhusu tarehe ya shule kufunguliwa iliyotolewa na baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema na sekta ya elimu nchini.

 

Taarifa hiyo imeenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikieleza kuwa shule zitafunguliwa tarehe 21 Septemba 2022 jambo ambalo sio sahihi na hakuna muongozo wala maelekezo hayo.

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekanusha uvumi huo leo tarehe 3 Septemba 2022 wakati akizungumza na wajumbe wa Bodi ya skuli ya Ole Sekondari iliyopo katika mkoa wa Kusini Pemba wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mjini Pemba.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa ratiba ya kufunguliwa shule ipo vilevile kwa mujibu wa waraka wa elimu Na 2 wa mwaka 2022 kuhusu mihula ya masomo uliotolewa na Kamishna wa elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Lyabwene Mtahabwa.

 

“Naomba mpuuze jambo hili kwanza aliyesambaza anatumia nembo ya kampuni moja ambayo kampuni hiyo haijui na haihusiki na tangazo hilo, kwahiyo hakuna maelekezo yoyote zaidi ya yale yaliyotolewa na kamishna wa elimu” Amekaririwa Waziri Mkenda

 

Kuhusu mageuzi ya elimu, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inafanya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 pamoja na mapitio ya mitaala ili kuboresha sekta ya elimu.

 

Amesema kuwa Tanzania Visiwani (Zanzibar) na Tanzania Bara zinafanya kwa pamoja mapitio hayo kwa karibu ili kupata mawazo ya wadau wa elimu na wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliyeitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inaboresha elimu hususani kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wakuwa na elimu ufundi na elimu ujuzi.

Na Mathias Canal, WEST-Pemba, Zanzibar

Leave A Reply