Waziri wa Ujenzi Amsimamisha kazi Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Eng. Andrea Kasamwa kwa kushindwa kusimamia urejeshwaji wa miundombinu ya barabara na madaraja katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi na kupelekea barabara kuu zinanounganisha wilaya hiyo na maeneo mengine kufungwa.
Waziri Bashungwa akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi ameshuhudia urejeshwaji wa barabara ya Liwale – Nangurukuru iliyosombwa na maji ikisimamiwa na Mtaalam mwenye taaluma ya Falsafa kwa kusaidiwa na Wananchi wakati Mkandarasi akiwa hayupo eneo la Kazi.
Bashungwa amechukua hatua hiyo tarehe 06 Machi 2024 wakati akikagua mindombinu ya barabara katika Wilaya ya Liwale na kutoridhishwa na usimamizi wa kazi inayofanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Lindi.
“Haiwezekani sisi tutoke Dodoma hadi huku Liwale kutokana na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara iliyopo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelazimika kutoa Helikopta yake tufike huku, lakini hapa site hakuna Mkandarasi, mnaweka mtu aliyesoma falsafa kusimamia kazi ya ujenzi wa barabara”, ameeleza Bashungwa.