Waziri wa Ulinzi Alivyofunga Mazoezi ya Medani ya Ushirikiano Kati JWTZ na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China
Pwani 12 Agosti 2024: Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) jana alifunga mazoezi ya pamoja yaliyokuwa yakifanywa kwa ushirikiano wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China.
Katika hitimisho hilo, Waziri Tax aliambata na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda na viongozi wengine wa ngazi za juu wa JWTZ na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China, Waambata wa majeshi rafiki na wageni wengine waalikwa kutoka sehemu mbalimbali.
Katika mazoezi hayo ambayo malengo yake makuu yalilenga kupambana na ugaidi na kuwaokoa watu mashuhuri vikundi vya makomandoo vikiwa uwanja wa shabaha kwenye Kambi ya Mapinga mbele ya mgeni rasmi vilionesha umahiri wa kulenga shabaha kwa kutumia silaha ndogo za kijeshi na magari vita (deraya).
Akizungumza baada ya kushuhudia maonesho hayo Waziri Tax aliyapongeza mazoezi hayo ya ushirikiano na kusema ushirikiano huo umeongeza kituo kikubwa kwa majeshi yote mawili kwakuwa kila upande kulikuwa na vitu wao ndiyo mahiri hivyo kubadilisha ujuzi na wenzao. Waziri huyo aliendelea kusema;
“Ushirikiano huu ulioanzishwa na waasisi wa mataifa haya mawili Tanzania na China, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung na kuendelezwa na marais wetu waliopo madarakani Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa China Xi Jinping ambao nao wanastahili pongezi kwa kuuenzi ushirikiano huu”. Alisema Waziri Tax.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda alianza na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha jeshi kuwa na vifaa vya kisasa nalo kuwa la kisasa zaidi.
Akielezea manufaa yaliyopatikana kwenye mazoezi hayo ya pamoja kati ya JWTZ yapo mengi sana lakini kuwa ni hili la ushirikiano na kuendelea kusema;
“Tunafahamu Tanzania na China tunaushirikiano mzuri wa muda mrefu ulioanzishwa na waasisi wa mataifa yetu haya mawili, Mao Tse Tung kwahiyo sisi hapo tunachofanya ni kama kuongeza tofari kwenye msingi uliojengwa na waasisi wetu hao.
“Lakini pia kwenye mazoezi haya tumeweza kutathmini uwezo wa jeshi letu, kwakuwa kwa kufanya mazoezi tu unaweza kuelewa uwezo wa jeshi, naamini umeona jinsi vijana walivyo na morali na kazi na umejionea jinsi walivyokuwa kwenye mazoezi ya kulenga shabaha ambapo ‘target’ walizowekewa wameweza kuzilenga zote tena kiufasaha.
“Kwenye haya mazoezi naweza kusema tumepata faida nyingi sana hizo ni mojawapo tu na naweza kusema mazoezi haya yameongeza hamasa kwa askari wetu”. Alisema Jenerali Mkunda.