The House of Favourite Newspapers

WCB WAMEITEKA BONGO FLEVA 90%

Image result for navy kenzo na sallam sk

WAHENGA wenzangu Bongo Flevani wanakumbuka Sterehe ya Ferooz, Nikusaidiaje ya Profesa Jay, Alikufa kwa Ngoma ya MwanaFA, Salome ya Dully Sykes, Mkuki Moyoni ya Afande Sele na nyingine kibao ambazo zilikuwa ‘hit songs’ lakini zina ujumbe. Mashabiki wa muziki walipata faidi mbili kutoka kwenye mashairi ya nyimbo hizi.

Moja walipata ujumbe, mbili waliburudika. Ngoma zilikuwa zinachezeka, zinaburudisha na zinaelimisha. Hii ni tofauti kidogo na vijana wa sasa wanaotokea Kundi la Wasafi Classic Baby (WCB). Asilimia kubwa ya ngoma zao hazina ujumbe kivile lakini mashabiki wametokea kuzielewa kwelikweli. Ulimwengu wa mashabiki umeleweshwa na midundo zaidi.

 

Wanaielewa midundo yao, kweli ukiisikiliza lazima upagawe. Kwenye nyimbo hizo hata wasipoimba vya maana bado wanapendwa. Wanasikilizwa na ndio zinazoongoza kwa sasa kusikilizwa.

Ukubali au ukatae lakini vijana hawa kwa sasa unaweza kusema ndio wenye muziki wao. Sikiliza Chombo ya Rayvanny, biti linapoonza kuna maneno fulani ambayo kimsingi hata hayaungi hata kuleta maana. “Olololo… Foundation, kwanja, nywele bei ya kiwanja, ndinga, mkwanja shopping mwendo wa kuchanga, Ngoma zao hazina maana lakini… sponsa, danga, uchune ukomeshe viranga, basi vimba, tamba, wakikuchamba…” Umenogewa eeeh? Kama nakuona unavyotikisa kichwa hapo ulipo.

 

Achana na hiyo, sikiliza Jibebe iliyowashirikisha Diamond Platnumz, Mbosso na Lava Lava; “Chaa…Ase go…ngoja njiseti, si walisusa nakula, fanya wainama kisha roteti tuwakunjishe na sura, leo shimo limetema meshinda bet (shinda bet), tuwaoneshe sinema wakina Fetty, asa jo njo, I like it, wema dachogodo, I like it, chinkolo chikologo, I like it, kono la sotojo, I like it, baby njoonjoo, I like it…” unauona utamu huo?

 

Sasa kama hiyo haitoshi sikiliza Kwa Ngwaru ya Harmonize ambayo ina ujumbe fulani wa mapenzi lakini kinachoibeba zaidi ni mdundo wake. Sikiliza Hodari ya Mbosso au Nipepee ambazo zinasifia mwanamke utaungana nami kwamba kuna maneno fulani hivi ambayo hayana maana sana lakini biti zake ni kali na vijana wana melodi nzuri.

Related image

KUNA CHA KUJIFUNZA

Muziki unakwenda na zama. Zama za zamani, ili uwe msanii ulikuwa unapaswa kujipinda kwa mashairi yenye ujumbe mkali zaidi kuliko kutegemea sana mdundo. Midundo ilikuwa na asilimia chache sana kumbeba msanii lakini kwa sasa mambo yamebadilika.

Ujumbe hauna nguvu sana. Kikubwa ni melodi na midundo. Hiyo ndiyo silaha zao kubwa. Zunguka kwenye kumbi mbalimbali za starehe kwa sasa, nadra sana kusikia ngoma za kizazi cha miaka ile hata kama wametoa ngoma mpya.

Related image

Asilimia tisini zinapigwa ngoma za WCB. Playlist za ma-DJ wengi huwa zinawapa nafasi kubwa sana Wasafi. Naamini hawafanyi hivyo kwa mapenzi yao binafsi bali wanafanya hivyo kutokana na mahitaji ya mashabiki.

Wanaamini ili wapate shangwe la kutosha, mashabiki wapate hisia za muziki mzuri basi upo WCB. Ukipanda Bajaj au nenda kwenye kijiwe cha madereva wa bodaboda, nyimbo za Wasafi zinachukua nafasi kubwa kuliko hata Singeli ambazo wakati fulani zilionekana kushika hatamu.

 

Wakongwe nao wameanza kubadilika, wameanza kuongeza nguvu kubwa zaidi kwenye midundo na maneno yasiyokuwa na ujumbe kivile.
Sikiliza Kadamshi ya Dully aliyomshirikisha Harmonize au Vunja Mifupa na Pagamisa za Profesa Jay utaona jinsi walivyobadilika!

Kumbe kuna kila sababu ya wakongwe kukubali mabadiliko kulingana na wakati kwani vinginevyo, unaweza kujikuta kila ngoma unayotoa inabuma!

Comments are closed.