The House of Favourite Newspapers

WCF  YAANZA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WAAJIRI WASIOJISAJILI

Meneja Matekelezo  wa WCF, Victor Luvena, akizungumza na waandishi wa habari.
Mmoja wa watuhumiwa wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) aliyefikishwa mahakamani.
Washitakiwa wakiwa chini ya ulinzi wa jeshi la Polisi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar.

 

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umewafikisha mahakamani waajiri wanne kwa kushindwa kujisajili na mfuko huo.

 

Waajiri hao ambao ni wakurugenzi watendaji, wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo wakikabiliwa na makosa mawili kila mmoja.

 

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Emilly Kilia, washtakiwa ni Wakurugenzi Watendaji wa LASAR LOGISTIC, Abushir Gure na Farhiya Hersiwarsame, Shafeek Purayil wakati mshtakiwa mwingine ni, Josephat Alexander ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kamanda Security Guards Co. Ltd.

 

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Victoria Nongwa, Kilia, alisema waajiri hao wametenda makosa  mawili ambayo ni  kushindwa kujisajili na kuwasilisha taarifa za shughuli wanazozifanya kwa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, ambapo ni kinyume cha Kifungu  cha 71 (1) (a) na 71 (4) cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi Sura ya 263  ya mwaka 2015.

 

Kosa la pili ni kushindwa kutoa taarifa kwa Ofisa wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambapo ni kinyume na Kifungu cha 8 (5) (c), kikisomwa pamoja na Kifungu cha 96 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura ya 263  ya mwaka 2015.

 

Imelezwa mahakamani hapo kuwa, kabla ya Mfuko  kuchukua hatua ya kuwafikisha  mahakamani, washtakiwa walipewa taarifa ya kutekeleza takwa hilo la kisheria katika tarehe mbalimbali, kati ya Septemba 2017 hadi Januari 2018 lakini walishindwa kutekeleza.

 

 

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, Meneja Matekelezo  wa WCF, Victor Luvena, alisema hatua ya kuwapandisha kizimbani waajiri hao ni mwanzo tu na kwamba Mfuko utachukua hatua kama hiyo kwenye mikoa yote Tanzania Bara.

 

Washtakiwa hao endapo watapatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo kisichozidi miaka mitano jela au faini isiyozidi shilingi milioni 50 au vyote kwa pamoja. Washtakiwa hao walitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa.

 

Comments are closed.