The House of Favourite Newspapers

We baba fanueliii!!!-18

0

ILIPOISHIA

“Heheh! Haloo…”

“Sawa! Subiri!”

Alichokifanya baba Fanueli ni kumsogelea kisha kutoa simu yake mfukoni, akaenda sehemu ya picha na kuzifungua zile picha alizotumiwa na mzee Paulo kisha kumuonesha, mama Zubeda akashtuka mno.

“Eeeh!” alijikuta akihamaki.

“Usihamaki! Kama ulivyokuja kuniharibia kwa mke wangu! Na mimi nakuharibia ili tuwe ngoma droo,” alisema baba Fanueli na kuanza kuondoka, mama Zubeda hakuweza kubaki, akaanza kumsogelea mzee huyo na kuanza kumuomba asifanye alichotaka kufanya, cha zaidi, akapiga magoti na kuanza kulia kama mtoto. Watu wote wakashangaa.

TAMBAA NAYO

Wewe si unajiona mjanja….”

“Naomba unisamehe…nipo chini ya miguu yako….”

“Hakuna kitu kama hicho! Wewe si ndiye siku ile ulikwenda kunifitinisha na mke wangu! Sasa zamu yako imefika,” alisema baba Fanueli.

“Baba Fanueli, naomba unisamehe…”

Watu wachache walioliona tukio hilo wakabaki wakimshangaa mama Zubeda, hawakujua alikuwa akiomba msamaha wa nini kwa baba Fanueli kwani mwanaume huyo hakuwa na tatizo na mtu yeyote mtaani hapo.

“Nikusamehe kwani umefanya nini?”

“Naomba unisamehe tu…”

Baba Fanueli hakutaka kuelewa, alikuwa na hasira na mwanamke huyo, alikuwa tayari kumsamehe mtu yeyote yule lakini si mwanamke kama mama Zubeda.

“Jamani kwani kuna nini?” aliuliza mwanamke mmoja, naye alikuwa kama mama Zubeda, mbeyambeya.

“Hata mimi nashangaa….” alisema baba Fanueli.

“Eti mama Zubeda kuna nini?”

“Mwambie anisamehe.”

“Kwani kakufanya nini?”

“Niombee msamaha….”

Baba Fanueli hakutaka kubaki mahali hapo, jinsi watu walivyokuwa wakikusanyika, akahisi kwamba kuna kitu kingeweza kutokea, akaangalia watu waliokuwa wamekusanyika pale, hakukuwa hata na mwanamke aliyetembea naye, hakutaka kubaki, alichokifanya ni kuondoka kurudi nyumbani, mama Zubeda hakubaki, akaanza kumfuata.

“Wewe Baba Fanueli wewe…..” aliita mama Fanueli huku akimshangaa.

“Na wewe unasemaje?”

“Jamani! Kwani tumegombana, mbona unaitikia kama tupo vitani!”

“Aya! Niambie unataka kusemaje!”

“Umemfanya nini mama Zubeda?”

“Kwani nimemfanya nini? Mbona sijamfanya kitu.”

“Nimesikia amekupigia magoti huko mtaani!”

“Sasa yeye si na umalaya wake, yeye si ndiye aliyekuletea umbeya, sasa nimemkomesha.”

Wakati wakizungumza hayo, naye mama Zubeda huyo akafika, alikuwa akilia huku akiendelea kumuomba msamaha baba Fanueli lakini mwanaume huyo hakutaka kusikia lolote lile.

“Jamani! Kwani kuna nini?”

“Umuulize huyo shoga yako!”

“Eti shoga’ngu, kuna nini?”

“Naomba mumeo anisamehe!”

“Akusamehe umefanya nini?”

“Mwambie anisamehe tu.”

“Kwani umefanya nini?”

Mama Zubeda hakutaka kujibu swali hilo, aliendelea kusisitiza kwamba asamehewe kwa kile kilichotokea. Baba Fanueli hakutaka kukubali, kila alipokumbuka jinsi mwanamke huyo alivyotaka kuivunja ndoa yake kisa tu alibambwa akiwa na mwanamke mwingine, alizidi kupandwa na hasira zaidi.

“Nakwenda kwa mumeo, wewe si ulimwaga mboga, sasa mimi namwaga ugali,” alisema baba Fanueli, mama Zubeda akaongeza kilio.

Baba Fanueli hakutaka kubaki nyumbani hapo, simu yake ilikuwa mkononi na yeye huyo akaondoka zake.

Mama Zubeda hakubaki nyumbani hapo, akamfuata baba Fanueli. Bado aliendelea kusisitiza apewe msamaha kwa kilichotokea. Alimfahamu mume wake, alikuwa mtu mwenye hasira kali ambaye siku zote alimwambia asimsaliti kwani angemuua.

“Mume wangu ataniua, naomba unisamehe….”

“Sasa akikuua si ndiyo vizuri!”

“Naomba unisamehe.”

“Yaani mwanamke mzima, eti unatembea nje ya ndoa, hivi mumeo hakutoshi?”

“Ananitosha!”

“Kilichokufanya kumsaliti?”

“Tamaa tu, naomba unistiri.”

“Kukustiri siwezi, lazima na mimi nikakinukishe ili moyo wangu ufurahi!”

“Naomba unionee huruma, nitakwenda wapi mimi jamani!”

“Si utakwenda kwa mchepuko wako! Au mshaachana?”

“Naomba usiniaibishe mwenzio, naomba unistiri baba Fanueli.”

“Hakuna hiyo! Tana nakumbuka dakika chache zilizopita ulinijibu shombo sana, tena ulijiamini sana, sasa nakwambia hivi, siwezi kukusamehe na iwe isiwe lazima mumeo azione picha zako,” alisema baba Fanueli huku kwa kumwangalia tu, alionekana kumaanisha.

Wala hawakuchukua muda mrefu, wakafika nyumbani kwa mama Zubeda, alichokifanya ni kuingia ndani bila kugonga hodi, alipofika sebuleni, akamkuta baba Zubeda akiwa kajaa tele. Mama Zubeda naye akaingia huku akitetemeka.

Leave A Reply