The House of Favourite Newspapers
gunners X

We baba fanueliii!!!-22

0

ILIPOISHIA

“Ndiyo!”

“Ngoja nikajiandae, nikawaandae na mashosti wengine twende, tena tuvae na madela yetu ya sare.” TEMBEA NAYO

Walitaka kwenda kumfumania, taarifa alizopewa kwamba shoga’ake ambaye alimpa umbeya ndiye aliyethubutu kutembea na mumewe.

Hakutaka kubaki nyumbani, ilikuwa ni lazima kwenda kumfumania pamoja na wanawake wenzake wa mtaa.

Wakavaa madela maalum ambayo huwa mara kwa mara wanayatumia kwenda kufumania au hata kumsuta mtu.

“Kumbe mwanamke mwenyewe ni mama Zubeda?” aliuliza mwanamke fulani hivi, kwa kumwangalia tu ungegundua kwamba alijipanga kwenda kumfumania mtu.

“Ndiyo!”

“Lakini nasikia ni shoga yako, si ndiyo?”
    “Ndiyo! Yaani mpaka nimeshangaa ananisalitije jamani!”

Walikuwa kumi, wakaondoka na kuelekea Manzese, mama Halima alikuwa kimbelembele kwani yeye ndiye aliyekuwa akifahamu mahali gesti ile ilipokuwa.

“Jamani tuwahini…wasije wakaondoka bure,” alihimiza mama Halima.

Ndani ya dakika kadhaa wakawa wamekwishafika Manzese, wakapitapita kwenye vichochoro mpaka walipofika mbele ya gesti moja, wakaingia ndani mpaka mapokezi, hata watu waliokuwa nje ya gesti hiyo wakipiga stori, waliwashangaa.

“Tumekuja kufumania,” alisema mama Halima bila kumung’unya maneno.

“Jamani! Sasa ndiyo mmekuja kishari?”

“Tangu lini umeona watu wanaofumania wanakuja kiamani? Tuambie wapo chumba kipi?”

“Akina nani?”
    “Tuliokuja kuwafumania.”
    “Jamani mbona siwaelewi?”

“Kuna mwanaume alichukua chumba hapa, kavaa shati jeupe na suruali ya kijivu, yupo chumba kipi?”

Dada wa mapokezi alipowaangalia wanawake wale, hawakuonekana kuja na amani, walikaa kishari na walichokihitaji ni kuoneshwa chumba tu. Hakuwa na jinsi, akawaonesha chumba. Wakaelekea huko.

“Jamani hebu nishaurini, nimfanye nini huyu malaya wa kuchukua wanaume wa watu?” aliuliza mama Fanueli.

“Subiri shosti, maamuzi ya ghafla yatapangiwa chumbani, cha msingi tuombe Mungu tuwafume.”

Walipokifikia chumba hicho, mama Fanueli akaanza kugonga mlango, baba Fanueli ambaye alikuwa ndani hakuonekana kuhofia chochote kile, akaufungua mlango, macho yake yakatua katika kundi la wanawake, wakiongozwa na mkewe.

“Hebu pisha huko…” alisema mama Fanueli huku akimsukumia mumewe ndani.
Wote wakazama ndani, wakamkuta mama Zubeda akiwa kitandani, kajifunga khanga moko tu, alipowaona wanawake hao wameingia, akashtuka, akajiweka vizuri, hata kabla hajafanya chochote, wanawake wale wakajifunga khanga vizuri.

“Eeeh! Aya wewe malaya ndiyo umefanya nini? Wewe si umeolewa na mumeo, nini kimekufanya kutembea na mume wangu?” alisema mama Fanueli, hata kabla hajajibiwa, mwanamke mwingine naye akaingilia.

“Halo halo….eti mwanamke mtu mzima unatembea na mume wa mtu, hivi kwani wanaume wamekwisha? Halafu kutwa kujifanya rafiki, rafiki gani mnafiki?” alisema mwanamke mwingine, hata kabla hajamalizia maneno yake, mwingine akaingilia.

Ilikuwa ni kupokezana tu, kila mmoja alimsuta kwa maneno yake ya kejeli, kila lililoongelewa hapo, mama Zubeda alikuwa kimya tu amejiinamia.

“Na wewe mwanaume, hivi sikuridhishi? Hivi na mimi nikiamua kutembea na wanaume wengine utajisikiaje? Kuna kipi kipya alichokupa huyu mwanamke?” aliuliza mama Zubeda. Baba Fanueli hakuwa na jinsi, akaanza kuomba msamaha.

Kwa mara ya kwanza baba Fanueli alifumaniwa, pamoja na kucheza mechi nyingi za ugenini, hakuwahi kufumaniwa hata moja.

Alikuwa na kila sababu za kumuomba msamaha mkewe na kuanza maisha upya.

Moyo wake haukuwa mgumu, akajifunza, akaahidi kutokutembea nje ya ndoa kwani kwa kile kilichotokea, alikubali kwamba za mwizi huwa arobaini.

Kutokana na aibu kubwa aliyokuwa ameipata, akamwambia mkewe wahame mtaa, wahamie katika nyumba yao iliyokuwa Mbagala, wakahamia huko.

Huku walipotoka, mama Zubeda hakuwa na amani, kila siku alikuwa mtu wa kujisikia aibu tu, hata akikuta watu wakizungumza na kucheka, alihisi anazungumziwa yeye.

Stori zilipomfikia mumewe, hakutaka kumkawiza, akamwandikia talaka tatu na kumuacha, hiyo ikawa fundisho kwa wanawake wengine wa mtaa.

Kwa kuwa alikubali kubadilika, baba Fanueli hakutaka kuendelea na wanawake wengine, akina Fatuma, Tunda na wengineo, wote akaachana nao, akataka kuwa karibu na mkewe tu.

“Umalaya haufai, utauona mzuri kama haujabambwa, ila ukibambwa, ni aibu kubwa sana,” alisema baba Fanueli, alikuwa akiwaambia wanaume wenzake.

“Ulipatwa na nini?”

“Hapa naizungumzia mvua iliyoninyea, yamenikuta, na ninaapa kutokurudia,” alisema baba Fanueli.

“Ila nasikia ulikuwa na vitoto vingine bwana.”
“Vyote nimeachana navyo, sitaki kusikia habari ya vitoto tena, havina ishu, vinakuchuna usiku na mchana, uvilipie kodi, uvinunulie chakula, hakuna hata kula raha na mkeo, sasa bora niachane navyo tu,” alisema baba Fanueli, kweli alidhamiria na kuanzia kipindi hicho, hakutaka kusikika mambo ya wanawake, yeye na mkewe, mkewe na yeye.

MWISHO

Leave A Reply