The House of Favourite Newspapers

We Miss Them!

0

WE miss them so much (tumewamisi mno)! Ndivyo wasemavyo Watanzania walio wengi wakati huu zikiwa zimesalia takriban siku 20 kumalizika kwa mwaka 2021; mwaka unaoelezwa kutawaliwa na machozi kila kona kutokana na vifo vingi vya viongozi, watu mashuhuri, mastaa, ndugu, jamaa na marafiki, Gazeti la IJUMAA lina ripoti kamili.

Mwaka 2021 uligubikwa na mfululizo wa vifo vya watu maarufu nchini tangu Januari hadi miezi ya katikati na mwishoni kidogo huku vikigusa nyanja zote za siasa, sanaa, sekta ya umma na viongozi wa dini kiasi cha kuacha maumivu makali mno kwa wafiwa nchini Tanzania.

VYANZO VYA VIFO

Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA ulibaini kwamba, vifo vingi vilitokana na vyanzo tofauti; vingine vilidaiwa kutokana na mlipuko wa janga la virusi vya Corona au UVIKO-19, magonjwa yasiyoambukiza kama presha na mengine, ajali na kwa upande wa wanajamii, vifo vingi vinatajwa kutokana na ukatili wa kijinsia, wivu wa mapenzi na uhalifu mwingine.

VINGOZI WAKUBWA

Kubwa kuliko, vifo hivyo viliwachukua viongozi wakubwa nchini akiwemo aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk John Pombe Magufuli kilichojiri siku ile ya Machi 17, 2021 na kugusa Watanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na Gazeti la IJUMAA wanasema hilo ndilo tukio kubwa zaidi kwa mwaka 2021 ambalo litawachukua Watanzania muda mrefu kulisahau kwani lilijiri wakati kiongozi huyo bado angali madarakani kwa miaka mitano na miezi mitano; kabla halijawahi kutokea tukio kama hilo.

WANAMMISI MAGUFULI

Watu hao wanakiri waziwazi kwamba, bado wanammisi Magufuli kwa namna ya uongozi wake na mambo aliyowafanyia.

Wakati mwaka 2021 unaingia, nusu ya pili ya mwaka uliotangulia wa 2020 ulikuwa umeshuhudia vifo mfululizo vya watu mashuhuri wakiwemo wabunge watatu akiwemo aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Augustine Mahiga.

Wengine walikuwa ni aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Gertrude Lwakatare na aliyekuwa Mbunge wa Sumve, Richard Mganga Ndasa.

Wengine mashuhuri walioaga dunia mwaka huo ni pamoja na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Waziri Mstaafu Arcardo Ntagazwa, Augustino Ramadhani, Nsa Kaisi, Bakari Mwapachu, Dk Masumbuko Lamwai, Askofu Anthony Banzi, Asha Muhaji na Khalifa Ilunga (C-Pwaa) aliyekuwa msanii maarufu wa Bongo Fleva.

Kuingia mwaka 2021, ndipo kukawa na mwendelezo wa vifo na machozi kila kona kiasi cha watu kujiuliza kulikoni?

WABUNGE

Misiba mingine ilikuwa ya wabunge wawili, walioaga dunia kwa sababu tofauti; Martha Umbulla kwa kuugua na Atashasta Nditiye kwa ajali ya gari.

WACHUMI

Usiku wa wa kuamkia Februari 22, 2021, Tanzania ilipoteza wachumi wawili bora zaidi; Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile (mume wa Vicky Kamata).

WANASHERIA

Wakati huohuo, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kilitoa orodha iliyoonesha takriban dazeni ya wanasheria waliopoteza maisha tangu kuanza kwa mwaka 2021; taarifa hiyo ilitolewa na Rais wa TLS, Rugemeleza Nshala.

Tasnia ambazo zilionekana na misiba kila uchao ni kama vile wanasheria, waandishi, viongozi wa dini na wanasiasa ambao kazi zao zinafanana kwa vile wanatakiwa kukutana na watu mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Vifo vingine vya mapema mwaka 2021 ni pamoja na kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Usafiri wa Mwendokasi (Udart), David Mgwassa kisha kilifuatiwa na kifo cha aliyekuwa Naibu Kamishina wa Jeshi la Magereza, Julius Sang’uti.

Kifo kingine cha mwanzoni kabisa kilikuwa cha Mwandishi na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Prudence Karugendo kikifuatiwa na kile cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga.

Siku ile ya Januari 22, 2021, alifariki Padri wa Jimbo Katoliki Bukoba, Ireneus Mbahulira.

MAALIM SEIF/BALOZI KIJAZI

Ulipoingia mwezi Februari, jinamizi la vifo liliendelea ambapo vifo vya kushtua zaidi vilikuwa vya siku moja ya Februari 17, 2021 ambapo walifariki dunia viongozi wawili wakubwa; aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Mwingine aliyeaga dunia siku hiyohiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na kuacha mshangao kwa wengi.

Wakati wa kuagwa kwa Hayati Magufuli siku ile ya Machi 21, 2021, Jeshi la Polisi Tanzania lilinukuliwa likisema kuwa, takriban watu 45 walipoteza maisha kwenye mkanyagano wa kumuaga kiongozi huyo jijini Dar.

ANNA MGHWIRA

Baada ya hapo kuliendelea kuripotiwa vifo vingi vilivyoshtua kikiwemo kile cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliyefariki dunia siku ile ya Julai 22, 2021 katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha alikokuwa akipatiwa matibabu kwa tatizo la kupumua.

Vipo vifo vingine vilivyoliza wengi kama kifo cha aliyekuwa mwanachama wa Chadema na mwanazuoni, Profesa Mwesiga Baregu aliyefariki dunia Juni 13, 2021 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

MAWAZIRI

Pia kipo kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Elias Kwandikwa ambaye alifariki dunia Agosti 2, 2021 akiwa hospitalini jijini Dar. Kwandikwa ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ushetu Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga alikuwa amelazwa kwa matibabu katika moja ya hospitali jijini Dar.

Septemba 17, 2021 kiliripotiwa kifo cha aliyekuwa Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, William Olenasha ambaye alifariki dunia ghafla jijini Dodoma. Olenasha alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro Mkoa wa Arusha.

Agosti 17, 2021, pia aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba alifariki dunia jijini Dar kwa ugonjwa wa UVIKO-19 (corona) katika Hospitali ya Regency.

Agosti 5, 2021, aliyekuwa Waziri wa zamani, Charles Keenja naye alifariki dunia na wakati familia wakiwa bado wanatafakari, wakapigwa mshangao baada ya kuelezwa kuwa, mkewe naye alifariki dunia. Keenja na mkewe wote walikuwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Saifee jijini Dar wakipatiwa matibabu.

INJINIA MFUGALE

Machozi mengine ya kukumbukwa ni siku ile ya Juni 29, 2021 kuliporipotiwa kifo cha aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Injinia Patrick Mfugale. Mfugale atakumbukwa kwa kusimamia ujenzi wa barabara na madaraja zaidi ya 1,000 nchini.

MATAJIRI

Eneo la biashara nalo liliguswa na vifo kwa kiasi kikubwa ambapo viliripotiwa vingi vikiwemo kifo cha Mwenyekiti wa Kampuni za ASAS Group, Alhaj Faraj Ahmed Abri ambayye alifariki dunia Agosti 13, 2021.

Matajiri wengine waliotangulia mbele ya haki ni Bilionea Mathias Manga aliyekuwa mfanyabishara maarufu wa madini akimiliki Hoteli za Gold Crest zilizopo jijini Arusha na Mwanza na alikuwa anamikiki majumba kadhaa ya kifahari na Salum Humud Sumry aliyekuwa mmiliki wa mabsi ya Sumri yaliyopata umaarufu miaka ya 2000 mpaka 2010 ambaye alifariki dunia Agosti 9, 2021 jijini Dar.

Wengine ni Tanil Kumar Somaiya almaarufu Shivacom ambaye alikuwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu nchini Tanzania akibobea kwenye sekta ya mawasiliano na ulinzi. (Ultimate Security) na John Lamba wa Travertine Hotel ambaye alikuwa mmiliki wa Hoteli ya Travertine ya Magomeni-Mapipa jijini Dar.

Pia Julai 31, 2021, jumuiya ya wafanyabiashara ilimpoteza aliyekuwa mmiliki wa Peacock Hotel, Joseph Mfugale na Haroon Zakaria aliyekuwa mmiliki makampuni kadhaa ikiwemo Kories, Murzah Oil Mills, Zan Fast Ferries na Majipoa.

Pia yumo William Mollel aliyekuwa mmiliki wa hoteli kadhaa za kitalii ikiwepo Snow Crest.

WASANII

Mbali na C-Pwaa wapo wasanii mbalimbali walioaga dunia 2021 akiwemo Mzee Matata wa Kundi la Mizengwe linalorushwa michezo yake kupitia Runinga ya ITV. Mwingine ni mwigizaji Mzee Msisiri aliyefariki dunia Aprili 30, mwaka huu.

WATANGAZAJI

Pia wamo watangazaji ambao walitangulia mbele ya haki wakiwemo, Fred Fidelis au Fredwaa, Mukhisin Mambo, Gabriel Kanonga, Juma Ahmed Baragaza (JB), Mwalimu Kashasha na wengine.

MICHEZO

Kwenye tasnia ya michezo napo hakukubaki salama kwani waliondokewa na wadau wake kama Hans Pope, Said Hamad El Maamry, Alhaj Muhidin Ndolanga na wengineo.

STORI; WAANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply