The House of Favourite Newspapers

WEMA AIKIMBIA NYUMBA USIKU

NI majanga juu ya majanga! Wakati akiwa amedakwa kisha kuburuzwa mahakamani kwa msala wa kusambaza picha za faragha mtandaoni, mwigizaji Wema Isaac Sepetu anadaiwa kuikimbia nyumba ya kifahari aliyokuwa akiishi kwa madai ya kushindwa kulipia kodi, Ijumaa Wikienda linakupa habari kamili.

 

Ijumaa Wikienda lilielezwa kuwa, Wema ameikimbia nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Salasala jijini Dar hivi karibuni huku pia ikielezwa alikuwa kikwazo kwa majirani zake kutokana na tabia mbalimbali alizokuwa akizionesha kwa kipindi chote alichoishi hapo.

 

MAPAPARAZI WATINGA

Baada ya kuelezwa kuwa mrembo huyo ametimka usikuusiku katika nyumba hiyo, mapaparazi wetu walifika katika nyumba hiyo ili kujiridhisha kama ni kweli ambapo walipofika, walibaini ni kweli baada ya kuzungumza na majirani. Mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini alisema kuwa ni kweli Wema alihama usiku wa saa mbili.

 

“Nilikuwa natoka kazini nikaona gari linatoka ikiwa na vyombo, nikauliza kwa rafiki yangu aliyekuwa pale, akaniambia kuwa Wema anahama, duh tunashukuru kwa sababu wale marafiki zake walikuwa wana vurugu, utakuta usiku sana wanafungulia muziki kwa sauti ya juu hadi usingizi ulikuwa unakata jamani kuishi jirani na staa ni shida,” alisema jirani huyo na kuongeza:

 

“Hata Serikali ya Mtaa wetu imefurahia sana maana tulikuwa tunaisumbua kila siku kuhusu suala la Wema kuwa msumbufu mtaani. Wamekuwa wakimuonya, wakimuita kwa barua, lakini wapi akawa anagoma.”

MJUMBE USO KWA USO

Akizungumza na Ijumaa Wikienda uso kwa uso, mjumbe wa mtaa aliokuwa akiishi Wema wa Mbezi-Salasala, Maliko Mbuku alianza kwa kusema kuwa anamtambua mrembo huyo, lakini akaeleza jinsi alivyokuwa anashangazwa na tabia zake kwani hakuwa na ushirikiano kabisa na majirani wenzake hata litokee tatizo gani ni yeye na geti lake tu hivyo hata kuhama kwake hawajapata taarifa zaidi ya kuona akitoa vyombo na kuviweka kwenye gari.

“Mimi nilisikia tu kuna msanii amehamia kwenye mtaa wangu. Baada ya kufanya uchunguzi ndiyo nikagundua kwamba alikuwa ni Wema. “Lakini cha kushangaza ni kwamba tangu amehamia hapa hajawahi hata kuja kwangu kujitambulisha kama wanavyofanya watu wengine wanapokwenda kuishi ugenini ni lazima aende kwa viongozi wake wa Serikali wamjue ili kama kuna tatizo lolote tujue tunasaidianaje,” alisema Mbuku.

 

HATUA WALIZOMCHUKULIA…

Alipoulizwa kama uongozi walichukua hatua gani baada ya kuona Wema anaishi kwenye mtaa wao bila kwenda kujitambulisha, haya ndiyo yalikuwa majibu yake:

“Kiukweli sisi baada ya kuona hajaja kwetu kujitambulisha hatukuhangaika naye kabisa, lakini kuna mambo ya ajabu ambayo tulikuwa tunayasikia na kuona kutoka kwake, mle ndani alikuwa anaishi na marafiki zake wengi tena wa aina tofautitofauti, wanawake kwa wanaume, tena bora basi wawe wanakaa kistaarabu yaani ukipita usiku unasikia wamefungulia muziki kwa sauti kubwa huku na wao wakiimba kama vile wapo disko.

 

“Kwa hiyo tulikuwa tunapata malalamiko mengi kutoka kwa majirani zake na mara nyingi tulikuwa tukimpelekea barua za wito nyumbani kwake ukifika geti halifunguliwi zaidi kuna katobo pale getini kwao, mlinzi anatoka anachungulia pale kisha unaweka barua kwenye hicho kitobo yeye anachukua, lakini haitikii wito, mpaka ilifikia hatua tulikuwa tunataka tumfukuze kwenye mtaa wetu, lakini kwa bahati nzuri juzi saa mbili usiku wakati tunapita pale kwake tukaona anahamisha vitu vyake na kuviweka kwenye gari,” alisema Mbuku.

AMETIMKIA WAPI?

Ijumaa Wikienda lilifanya jitihada za kumtafuta Wema kupitia simu yake ya mkononi ili kujua alikohamia na pengine kujua sababu zilizomfanya ahame, lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Hata hivyo, kuna madai kuwa mrembo huyo ‘amerudisha mpira kwa kipa’ kwa kuhamia nyumbani kwa mama yake maeneo ya Sinza- Mori, Dar, madai ambayo Ijumaa Wikienda linaendelea kuyafanyia kazi.

 

TUJIKUMBUSHE

Alhamisi iliyopita, Wema alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar na kusomewa shitaka la kusambaza picha za faragha mtandaoni. Wema anadaiwa kujirekodi video za faragha na mpenzi wake anayefahamika kwa jina la Patrick Christopher ‘PCK’ ambaye pia anasakwa nchini kwa misala mbalimbali ikiwemo ya madawa ya kulevya.

 

BODI ILISHAMFUNGIA

Oktoba 26, Bodi ya Filamu nchini, ilitangaza kumfungia mwigizaji huyo kutojishughulisha na uigizaji kwa muda usiojulikana, kufuatia picha zake hizo zilizosambaa mtandaoni. Mapema Oktoba 26, kabla ya uamuzi wa huo, Wema aliomba msamaha kutokana na tukio hilo.

STORI: Memorise Richard na Neema Adrian, DAR

Comments are closed.