Siku Chache Baada ya Kukimbia Bastola kwa Nape, Hamorapa Anusa Kifo!

Hamorapa akitulizwa baada ya kutaharuki.

DAR ES SALAAM: Chuki! Zikiwa zimepita siku chache baada ya msanii chipukizi wa Bongo Fleva lakini mwenye matukio mengi, Athuman Omary maarufu kama Harmorapa, kukimbia baada ya kushuhudia mtu asiyefahamika akichomoa bastola na kumwelekezea Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye katika Viwanja vya Hoteli ya Protea, Oysterbay jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita alinusurika kifo, baada ya kijana mmoja kumtu pia chupa iliyojaa bia akimlenga kichwani lakini ikamkosa, wakati akifanya shoo kwenye Ukumbi wa Maisha Basement, Kijitonyama.

Mabaki ya chupa.

HALI ILIKUAJE KWANI?

Dayna Nyange , mmoja wa wasanii wanaofanya vizuri katika Bongo Fleva, alikuwa ameandaa shoo yake ndani ya ukumbi huo akiipachika jina la Usiku wa Komela na Harmorapa alikuwa mmoja wa wasanii waalikwa.

Mtuhumiwa akiwa hoi kwa kipigo.

Harmorapa ambaye amejipatia jina kubwa ghafla, baada ya kufanana kwa kiasi kikubwa kimuonekano na chipukizi mwingine kutoka Kundi la WCB, Abdulhan Rajab ‘Harmonize’, alikuwa ndiye msanii ‘mwenye jina kubwa’ baada ya Dayna Nyange, wengine wakiwa ni ma-underground.

SAA TISA KAMILI USIKU Kwa kawaida, ndani ya ukumbi huo wa burudani, huwa na matukio mengi ya kiburu
dani na katika shoo kama ya siku hiyo, huanza baada ya saa nane usiku, ambako wasanii wakubwa huanza kutumbuiza. Jumapili, saa tisa usiku, wakati shoo ya Komela, ikiwa imeanza, muda wa Harmorapa kupanda uliwadia, akiwa katika shoo akitumbuiza na wimbo wake unaotamba hivi sasa wa Kiboko ya Mabishoo, tukio la kusikitisha likajitokeza.

…akiingizwa kituoni Mabatini.

HIKI NDICHO KILICHOMPONZA HARMORAPA

Katika kibao hicho cha Kiboko ya Mabishoo, baadhi ya
mashairi yake yanasema… ”Tulikuwa wasafi kabla ya WCB, maneno yao machafu hayanivunjii sivi…,” Maneno hayo yalionekana kumkera kijana mmoja aliyekuwa miongoni mwa mashabiki, ambaye bila kujali athari amba zozingetokea aliinua chupa iliyojaa bia, iliyokuwa  haijafunguliwa na kumlenga msanii huyo, ambaye hata hivyo, akiwa hajui hili wala lile, alishtukia kishindo kikubwa cha mlio wa chupa iliyopasuka.

TAHARUKI UKUMBINI

Kishindo hicho cha chupa kiliibua taharuki kubwa ukumbini, huku muziki ukizimwa kwa muda na Harmorapa, aliyekuwa kama aliyechanganyikiwa kwa kutojua nini kilichoendelea, alichukuliwa haraka ukumbini na kwenda kuwekwa sehemu salama.

Mtuhumiwa akisachiwa na malinzi.

Wakati hayo yakitokea, walinzi wa ukumbi huo nao walimuwahi kijana huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja na kumpeleka eneo salama zaidi kwao, akiwa chini ya ulinzi lakini hata hivyo, mashabiki waliojawa na hasira, walishindwa kuvumilia na kuamua kumpa kipigo kikali, kilichomuacha na majeraha kadhaa, hasa mdomoni.

Kuona hivyo, walinzi wa ukumbi huo walimchukua kijana huyo na kumpakiza kwenye gari na kumkimbiza katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama, maarufu kama Mabatini, ambako baadaye, Harmorapa na meneja wake, Irene Sabuka pia walikwenda kutoa ushahidi.

MSIKILIZE MENEJA WA HARMORAPA

Irene akizungumza wakati akiwa kituoni hapo, aliliambia Risasi Mchanganyiko, kuwa amesikitishwa na kitendo hicho kwani hajui kwa nini watu wanaumizwa na harakati za kijana huyo mdogo, anayejitafutia maisha kama wao walivyoanza kutoka kimuziki.

“Ninachokiona hapa ni chuki tu ambazo hazina maana, watu wanaonekana wanakereka sana kumuona huyu kijana akifanya vizuri, wangemuacha tu na yeye ajitafutie maisha yake kwa sababu kila mmoja alianza hivihivi.”

Kwa upande wake, Harmorapa alisema kitendo hicho kilimuumiza sana, lakini hajavunjika moyo, atakaza buti kuliko zamani hadi kieleweke.

“Kitendo kile kilinishtua, sikutegemea kama kingetokea, kilinitoa katika mudi kabisa, hata hivyo hakiwezi kunifanya nikate tamaa maana bado niko ‘strong’ na kama hawajui basi ni kuwa wananiongezea ari ya kupambana zaidi,” alisema.

Wanahabari wakipiga picha mabaki ya chupa.

Hamorapa akitulizwa na wasanii wenzake.    

Toa comment