The House of Favourite Newspapers

Wema aongeza nguvu kumzima Mondi!

MAMBO yamezidi kuwa moto! Lile bifu kati ya mastaa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, Rajab Abdul ‘Harmonize’ dhidi ya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ limechukua sura mpya baada ya mrembo Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ kuonesha upande na kutia neno, Ijumaa Wikienda linakupa mchapo kamili.

 

TULICHAMBUE BIFU KWANZA

Kiba na Diamond au Mondi, bifu lao ni la muda mrefu ambapo lililipuka upya wiki iliyopita baada ya Mondi kumualika Kiba kwenye shoo yake ya Wasafi Festival iliyofanyika usiku wa juzi Jumamosi kwenye Viwanja vya Posta-Kijitonyama jijini Dar.

 

Kwa upande wa Harmonize au Harmo, naye amejikuta akiingizwa kwenye bifu hususan na mashabiki ambao hawampendi Mondi hivyo kitendo cha yeye kujitoa Wasafi, kimetafsiriwa kuwa ni uadui na sasa huko mitandaoni ni vita ya maneno, ‘Team’ Mondi vs Harmo au Konde Boy.

TURUDI KWA MADAM SASA

Akizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda kuhusu mtazamo wake katika ishu ya Mondi na Kiba, Wema ambaye ni staa wa sinema za Kibongo alisema hakuna sababu ya kumulika tochi kwani ukweli ulio wazi, Kiba anajua zaidi ya Mondi.

NI MPENZI WA NYIMBO ZAKE…

Wema alisema, alianza kupenda nyimbo za Kiba tangu kitambo na hata Mondi analijua hilo na nyimbo zake anazipenda na anaweza kusikiliza wakati wowote.

“Unajua watu hawaelewi, mimi siwezi kuficha hisia zangu hata kidogo, ni kweli kabisa nauelewa muziki wa Kiba, uzuri hata Diamond mwenyewe anafahamu hilo na kingine ni vyema kujiachia ni wapi unapenda na unapata hisia kali unaposikiliza muziki wake,” alisema Wema.

AZIDI KUTIRIRIKA

Staa huyo aliongeza kuwa, pamoja na kuwa watu wanaongea kuhusu mastaa hao, lakini Kiba ni mwanamuziki na mtunzi mzuri sana wa nyimbo na nyimbo zake zinadumu kwa muda mrefu kwa maana hata kama wimbo ameuimba miaka kumi iliyopita, lakini bado ukisikiliza leo utapata burudani.

“Ni hivi, nitaendelea kuwa shabiki siku zote wa Kiba, hakuna chochote ambacho kitanifanya nisifanye hivyo maana kizuri kinajiuza na kama kuna mtu atachukia kwa hilo, atakuwa siyo muelewa kwa sababu muziki ni hisia kali zilizopo ndani ya moyo wa mtu,” alisema Wema.

KWA HARMO PIA

Mbali na Kiba, Wema ameonekana kumuunga mkono pia Harmo kwani mara kadhaa amekuwa akimsapoti kwa kucheza nyimbo zake, jambo ambalo limekoleza harakarati za kumzima Mondi.

Mara kadhaa Wema amekaririwa akimsifia Harmo na kutamka wazi kuwa kwa sasa anamzidi Mondi kwa ubora wa muziki wake.

Kitendo cha Wema ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa Mondi kuonekana kumuunga mkono kila ambaye anakuwa na tofauti na jamaa huyo, kimekoleza mashabiki kumsema vibaya Mondi mitandaoni.

“Safi sana Madam, huyu Mondi mwisho wake ndiyo huu, lazima tummalize, yeye si anajifanya anajua sana, sasa kwa nguvu hii kuna nini tena,” aliandika mitandaoni shabiki mmoja.

ANGUKO LA MONDI LATAJWA

Kama hiyo haitoshi, mashabiki wengi waliozungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda, Jumamosi iliyopita, walisema anguko la Mondi litajidhihirisha kwenye shoo ambazo wapinzani wake hao watakapofanya shoo zao.

Jumamosi iliyopita, Harmo alitarajia kuangusha bonge la shoo katika Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga huku Wasafi wakifanya yao Viwanja vya Posta- Kijitonyama jijini Dar ambapo mashabiki walikuwa na shauku ya kuona ni nani atamfunika mwenzake.

“Tutaona sasa, Mondi si kajaza wasanii wengi wa ndani na nje ya nchi, sasa sikilizia Jeshi (Harmo) atakavyofanya balaa huko Shinyanga,” alisema Kidumu, mkazi wa Sinza jijini Dar.

Aidha, Kiba naye anasubiriwa kwa hamu na mashabiki hao kwani wameeleza kufurahishwa na utambulisho wa ziara za matamasha yake alizozipa jina la Unforgettable Tour ambayo wanaamini itaifunika Wasafi Festival.

“Tutaona, Kiba tayari katambulisha Unforgettable Tour itakayoanza mwakani, huyu Mondi ataponea wapi kwa mfano, huku Harmo anakimbiza kule Kiba ana shoo za tour kama ambazo Wasafi watakuwa wanafanya,” alisema Amina Kinjeo, mkazi wa Buguruni, Dar.

TUJIKUMBUSHE

Bifu la Kiba ambaye ameachia wimbo mpya wa Mshumaa na Mondi lilitajwa kusababishwa na Wimbo wa Lala Salama ambao Mondi alidaiwa kutoa mashairi ya mwenzake huyo baada ya kurekodi naye. Tangu hapo, wawili hao hawajawahi kuiva huku wakitajwa kufanyiana figisufigisu za hapa na pale katika suala zima la mafanikio ya kimuziki.

Kwa upande wa Harmo anayekimbiza na Wimbo wa Uno, yeye bifu limekuzwa zaidi na mashabiki baada ya kufunguka kuwa uongozi wa Mondi umemtaka alipe shilingi milioni 500 kama fedha za kuvunja mkataba baada ya kujitoa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na Mondi anayekimbiza na wimbo mpya wa Baba Lao.

Tangu hapo, watu wamemtafsiri kama Mondi hampendi bwa’mdogo huyo hivyo sasa kumuwashia moto huko mitandaoni.

Kwenye mahojiano ya hivi karibuni, Harmo alikiri kuwa yeye na memba wa Wasafi kwa sasa mawasiliano yao si kama ya zamani kwani kibinadamu huenda kwa kila atakayejaribu kuwasiliana naye ataonekana msaliti.

 

STORI: IMELDA MTEMA, DAR

Comments are closed.