The House of Favourite Newspapers

WEMA; KAMWE SHERIA HAISAMEHI 7 MARA SABINI

 

Wema Sepetu

UMEFIKA wakati Wema Sepetu achunguzwe akili kwa sababu tabia zake zinatia mashaka huenda kuna shida kichwani mwake.  

 

Likijulikana tatizo linalomkabili ni rahisi kumsadia kuliko kumuacha aishi kama gari lililopoteza mwelekeo; Wema wa juzi, jana na kesho huwezi kumuwekea dhamana. Kituko cha picha na video chafu alichokifanya hivi karibuni kinafikirisha zaidi hasa pale unapouangalia utashi wa kibinadamu ambao kimsingi ndiyo unaomtofautisha mtu na mnyama.

 

Iweje Wema awe faragha na mpenzi wake, ajirekodi uchafu wake halafu aje awaoneshe ndugu, jamaa na wazazi wake; tena kwa hiyari yake, kisha baadaye aangue kilio na kuomba msamaha kwa kuwaonesha uchafu huo?

 

Kama lipo jibu la hoja hii basi hakuna mashaka kwamba msichana huyo ‘dishi’ la kichwa chake limecheza au wale wapambe ‘waliomshikia akili’ wamewehuka. Haiwezekani watu wazima wenye maarifa yao wavunje sheria kila wakati halafu suluhisho lao liwe ni kuitisha vyombo vya habari na kuomba msamaha kwa machozi ya kinafiki.

 

Sheria Haisamehi Saba Mara Sabini; Wema na hao waliopinda akili wanapaswa kujua hili, ndiyo maana ikithibitika umeiba hata kwa mara ya kwanza unahukumiwa kufungwa. Machozi hayajawahi kumsaidia mtu kuikimbia jinai.

 

Kwa kumwelimisha Wema ambaye naona hata vibaya kumpa heshima ya Umiss Tanzania aliopewa mwaka 2006 ni kwamba hata maandiko katika Kitabu Kitakatifu cha Biblia ambayo pengine ndiyo yanayomsukuma kuomba radhi, hayasemi mtu avunje sheria za nchi hata mara sabini halafu asamehewe kihunihuni. TUSOME Mathayo 18: 21-22 maandiko yanasema hivi:

 

Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

 

Swali la Petro kwenda kwa Yesu halikuuliza kuhusu kuvunja sheria za nchi na maadili ya jamii, lilihusu makosa juu ya ndugu si vinginevyo. Kama Wema angelikuwa amemkosea mama yake mzazi au mjomba wake kama si dada wa tumbo moja angewaendea hao na kuwalilia machozi na mambo yakaisha.

 

Lakini kupiga picha za ngono na kuzisambaza mitandaoni hakuwezi kuishia kwenye vipaza sauti kwa mtu kutubu kisanii, labda niambiwe kuwa wasimamizi wa sheria za nchi yetu ni wajomba zake ndiyo maana alikwenda kuwalilia ili wasimb-uruze mahaka-mani akahukumiwa. Twende mbele na kurudi nyuma katika hili, pengine washauri wa Wema walimwambia: “Nenda haraka kaombe radhi wakubwa wakiona huwezi kuchukuliwa hatua.”

 

Nasema hivi kwa sababu sitaki kuamini kwamba washauri wa msichana huyu ni wajinga kiasi hiki; kwamba kosa wanalitengenezea ushahidi mapema ili kumuwezesha Wema atakapofikishwa kwenye sheria asiisumbue mahakama kwa kuwa ushahidi wa kukiri kosa ameshautoa mbele ya vyombo vya habari.

 

Siweki msukumo wa nini cha kisheria kifanyike juu ya wasanii wachache ovyo na Wema ambaye kiukweli sijisikii vizuri kumpa sifa yoyote ya uzuri, uigizaji mahiri kwa sababu tangu kaanza vioja vyake vya kijinga, ameshapoteza sifa za ubora. Ni Wema huyuhuyu aliyekuwa analilia upuuzi alioufanya juzi akiomba asamehewe amenusurika kufungwa hivi karibuni kwa kosa la matumizi na kuhifadhi dawa za kulevya.

 

Mwaka 2009 aliwahi kumfanyia vurugu msanii Steven Kanumba (Marehemu) akavunja kioo cha gari, alitiwa mbaroni na polisi lakini baadaye akasamehewa. Hilo halikumfanya akome, mwaka 2011 akamtusi mwanamuziki Rahem Nanji, ‘Bob Junior’ akaburuzwa mahakamani akahukumiwa kifungo cha miezi 6; akajiokoa kwa kulipa faini.

 

Sikio la kufa halikusikia dawa, akarudia kosa lingine la kumfanyia vurugu na kumtusi meneja wa hoteli moja jijini Dar, akakamatwa na polisi. Ukiacha hilo, mambo ya picha za ngono mitandaoni ndiyo usiseme; tangu zama za mapenzi ya Nasibu Abdul ‘Diamond’ mpaka sasa kwa hawa wanaume hamnazo anaosambaza nao video za ngono yuko vilevile!

 

Waswahili husema, asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu, huu ndiyo wakati wa wasanii wapuuzipuuzi kufunzwa na ulimwengu. Ni wakati wa vyombo vya kulinda sheria kusimama sawa ili maadili ya jamii yanyooke, mambo ya kuwaonea huruma wanaolia kinafiki hayafai.

 

Hakuna mtu aliyelia kwa hisia kali kama mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius wa Afrika Kusini akitubu mbele ya mahakama na umma kwamba alimuua mpenzi wake bila kukusudia lakini hakuachwa acheze na sheria kwa sababu alilia sana; leo hii yuko jela anatumikia kifungo cha miaka 5.

 

Wasanii wetu wa Kibongo wengi hawajaguswa na mkono wa sheria kwa sababu kuna viongozi wapambe sijui kwa maslahi ya nani wamekuwa wakijitokeza nyuma ya mashauri ya kisheria kuonesha utetezi wao kwa watuhumiwa.

 

Ndiyo maana leo tunashuhudia baadhi ya wasanii wakirekodi video za ngono tena wakiingiliana kinyume cha maumbile na kuzisambaza mitandaoni na kesho yake unasikia; ‘naomba msamaha’. Nalazimika kuamini kwamba hizi naomba msamaha zina maana nyingine kubwa zaidi ya tuijuayo ila kwa kuwa sijaifanyia utafiti wa kutosha na kupata data; acha ninyamaze, tukutane wakati mwingine!

RICHARD MANYOTA

Comments are closed.