The House of Favourite Newspapers

Wema Sepetu Aswekwa Ndani Hadi Juni 24

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemwamuru msanii wa filamu nchini na Miss Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu,  kukaa mahabusu kwa siku saba hadi Jumatatu ijayo, Juni 24, wakati akisubiri uamuzi wa mahakama kumfutia dhamana baada ya kukiuka masharti aliyopewa mahakamani hapo.

 

Hiyo imekuja ikiwa ni baada ya siku sita kupita tangu Mahakama hiyo ilipotoa amri ya kumkamata kwa kushindwa kuhudhuria kesi yake inayomkabili mahakamani hapo.

 

Wema ambaye ni mshindi wa Miss Tanzania 2006, amepandishwa gari la Magereza kutoka mahakamani hapo na kupelekwa gereza la Segerea ambapo inaelezwa kuwa atakaa hadi Juni 24.

 

Kesi yake itasikilizwa Juni 24, ambapo Mahakama itatoa uamuzi wa kufuta dhamana yake ama la. Amri ya kumkamata msanii huyo ilitolewa Juni 11, mwaka huu na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde, baada ya mrembo huyo wala mdhamini wake kushindwa kufika mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi inayomkabili.

 

Wema anakabiliwa na kesi ya jinai ya kuchapisha video ya ngono na kusambaza katika mitandao ya kijamii.

 

Comments are closed.