The House of Favourite Newspapers

WEMA SEPETU NA REKODI YA KUMILIKI MAGARI YA KIFAHARI

Wema Sepetu

 MAISHA ni safari ndefu isiyokuwa na likizo na katika maisha hayo kuna wakati mtu unapanda na kushuka, yaani safari ya maisha ni fumbo kubwa kwa kila binadamu. 

 

Unaweza ukawa unaishi vizuri leo ukiwa mwenye furaha na amani lakini ghafla kesho unajikuta ukiwa katika maisha ya shida na kilio kila kukicha, hayo ndiyo maisha! Katika ulimwengu wa mastaa nako kuna waliokuwa na maisha mazuri ya kifahari lakini leo wamekuwa wa kawaida na zile mbwembwe walizokuwa nazo kipindi hicho hazipo tena.

 

Kwenye makala haya tunakuletea mrembo aliyeshikilia taji la Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye katika rekodi inaonesha ndiye staa wa kike ambaye amewahi kutumia au kumiliki magari ya kifahari ndani ya miaka 10 mfululizo Bongo.

 

Kwa sasa Wema anatumia gari aina ya Toyota Crown Majesta lenye thamani ya shilingi milioni 14 za Kibongo ambapo anafunikwa na mastaa wengine wa kike tena wale wanaochipukia kwenye sanaa kwa sasa kama Lynn, Nandy, Lulu Diva na wengineo wenye magari ya kifahari.

 

Huwezi kuamini kama yeye ndiye yule ambaye amewahi kutumia magari ya kifahari kiasi kile lakini ndiyo maisha yenyewe kwani ndivyo yalivyo. Hapa chini ni aina ya magari ya kifahari ambayo Wema amewahi kuyatumia kabla ya kufikia kwenye maisha ya kawaida aliyonayo sasa.

TOYOTA LEXUS

Mwaka 2012 ulikuwa mzuri kwake ikiwa ni baada ya kudaiwa kununuliwa gari hilo na kigogo mmoja (jina linahifadhiwa) lenye thamani ya shilingi milioni 35 (sokoni milioni 28 hadi 35 za Kibongo). Licha ya kudaiwa kununuliwa gari hilo na kigogo, Wema hakudumu nalo kwa muda mrefu ikiwa ni baada ya kupata lingine (Toyota Mark X) na hilo kuamua kumpa mama yake kama zawadi.

TOYOTA MARK X

Baada ya kumpa mama yake Lexus, alivuta gari jipya aina ya (Toyota Mark X) ambalo alidai lilikuwa na thamani ya shilingi milioni 38 (kwa sasa sokoni ni milioni 28 hadi 35). Wema alisema ameamua kununua gari hilo ili kubadilisha mazingira.

AUDI Q7

Kwa mara ya kwanza Wema alianza kuon-ekana na gari hili mwaka 2013 katika Fukwe za Coco jijini Dar ambapo aliweka picha mtandaoni na kusema kuwa amepata ‘baby’ mpya ambaye yupo naye ufukweni. Hata hivyo, ilikuja kujulikana baadaye kuwa gari hilo alipewa na kigogo mmoja aliyekuwa akitoka naye kimapenzi kipindi hicho (jina linahifadhiwa) ambalo alimnunulia kwa bei ya shilingi milioni 80.

BMW 545i

Mwaka 2014 katika sherehe ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa ‘bethidei’ iliyofanyika alikokuwa amepanga zamani, Kijitonyama jijini Dar alizawadiwa gari hilo na meneja wake, Martin Kadinda. Baadaye gari hilo lilileta mgogoro baada ya aliyekuwa bwana’ke enzi hizo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kukataa kuwa Kadinda hawezi kulinunua kwani thamani yake ilitajwa kuwa ni milioni 56 wakati sokoni linapatikana kwa milioni 40 hadi 45.

NISSAN MURANO

Ndani ya sherehe hiyohiyo ya bethidei, aliyekuwa mpenzi wake, Diamond alimkabidhi Wema gari aina ya Nissan Murano lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 36. Diamond alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kumpongeza kwa siku yake ya kuzaliwa na kuweka wazi kuwa ameamua kumzawadia gari.

 

RANGE ROVER EVOGUE

Katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa mwaka 2015 iliyofanyika Millenium Towers, Kijitonyama jijini Dar, usiku huo ambao alisindikizwa na mastaa kibao wa filamu Bongo na watu mbali-mbali, Wema aliwatoa wageni waalikwa hadi nje ya ukumbi huo na kuwaonesha gari hilo ambalo alidai amejizawadia. Mwanadada huyo alisema gari hilo alilinunua kwa thamani ya shilingi 140 Kibongo.

STORI: GLADNESS MALLYA

NAVYKENZO! kutoka Banda La Uani Hadi Kumiliki Ghorofa

Comments are closed.