The House of Favourite Newspapers

WEMA WA SASA ANAFELI WAPI?

KWA takriban miaka kumi tangu mrembo wa Taifa, Wema Sepetu atwae Taji la Miss Tanzania hakuwahi kuchuja. Kama ni moto ulikuwa unawaka kila uchwao. Tangu mwaka 2006 grafu ya Wema ilikuwa inapanda tu.

 

Nyota ya mrembo huyu ilikuwa ni ya hali ya juu, alikuwa kila anachokifanya lazima kitaungwa mkono na mshabiki wengi sana ambao walikuwa na moyo wa kumfuatilia, yaani hao ni wale wa kufa au kupona, huwaambii kitu.

Nakumbuka Wema wa zamani alikuwa na wafuasi wengi zaidi mitandaoni kuliko msanii yeyote hapa Bongo. Wema alikuwa kila anapokatiza, iwe ni klabu au hata kwenye shughuli fulani kubwa basi anapoingia kila mmoja atatambua uwepo wake.

 

Wema wa zamani alikuwa kama uaridi vile, kila anayemzunguka lazima naye awe staa. Shoga wa Wema ilikuwa lazima azungumziwe. Mtu yeyote atakayeingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mrembo huyu, kama si maarufu atakuwa na kama ni maarufu basi umaarufu wake utaongezeka zaidi.

 

Utakumbuka jinsi alivyomuongezea kasi ya umaarufu marehemu Steven Kanumba wakati alipokuwa na uhusiano naye, usisahau kuhusu Yusuph Jumbe ambaye alikuwa mjasiriamali tu lakini alivyoonja tu penzi la Wema, akawa maarufu kwelikweli.

ALIMUONGEZEA KASI DIAMOND

Wema wa zamani alimuongezea kasi ya umaarufu Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, alipokuwa naye kila mtu alijua. Diamond alipata umaarufu zaidi baada ya kuwa na Wema, kazi zake zilifuatiliwa zaidi hadi pale alipoamua kujinasua na kuangukia mikononi mwa Mganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.

 

MUONEKANO UNACHANGIA?

Muonekano wa Wema umepitia kwenye madaraja matatu mpaka sasa; wembamba, unene na sasa wembamba tena. Shepu la Wema lilivyojaajaa lilimuongezea mvuto sana mrembo huyu mbele ya jamii, alikuwa mtu wa tofauti na watu wa kawaida. Lile umbo lake lilipendwa sana, lilikuwa linashtua.

 

Ilikuwa haihitaji uwe mtoto wa mjini kivile ili uweze kumtambua Wema pindi anapokatiza mahala hata kama ni usiku mnene. Suala la msingi la kuzingatia ilikuwa ni ‘lile lishepu’ lake kama vile la kuchora ambalo alikuwa nalo, ukiliweka akilini tu unakuwa umeshamjua.

 

Muonekano huu ulikuwa gumzo zaidi kwenye mitandao hata ukiona zile video zake ambazo amekuwa akizirusha kuonesha muonekano wake. Baada ya miaka mingi kupita Wema akiwa na lishepu kama lote, sasa mrembo huyu amejikondesha.

MVUTO KUPUNGUA

Amerudi kwenye muonekano kama ule wa 2006. Tukubali tukatae, kwa kawaida mwili wa mwanadamu siku zote unaongezeka kadiri mtu anavyokua. Hivyo unapokuwa umefika mahali umenenepa halafu ukakonda sana, hakika muonekano wako hauwezi kuvutia sana.

 

Angalau kama angekuwa amepungua kidogokidogo lakini kwa kupungua ghafla, muonekano wake umeleta picha ya tofauti sana. Ile shepu ambayo alikuwa nayo kwa muda mrefu kuondoka ghafla ni rahisi pia hata watu kupishana na wewe bila kukujua kama ilivyokuwa zamani hususan usiku.

 

Wema ambaye alichochea umaarufu wa Diamond, kwa sasa msanii huyo amemzidi umaarufu katika mtandao wa Instagram. Wema ana wafusi milioni 4. 9 wakati Diamond ana wafausi milioni 6.6 hivyo kuna kitu anapaswa kujifunza.

 

UKOMAVU WA UPEO

Kwa sasa inaonekana upeo wa Wema umekua, hivi karibuni ameonesha ukomavu huo katika risala yake aliyoitoa kwenye mkusanyiko wa watu. Amezungumza namna ambavyo amefelishwa na marafiki ambao wamekuwa wakimtumia na kumfanya ashindwe kupiga hatua.

Umaarufu wa Wema unapaswa kufanana na mafanikio, akijitambua na kuona alipofeli kisha akachukua hatua basi anaweza kurudi kwenye mstari!

Comments are closed.