LONDON, England
KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger amesema hakuna tatizo lolote kati yake na mshambuliaji wa timu hiyo, Alexis Sanchez.
Mshambuliaji huyo wa Arsenal alionyesha kukasirika wakati alipotolewa uwanjani kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Swansea, juzi Jumamosi.
Staa huyo raia wa Chile alionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo huo baada ya kufunga bao moja na kutengeneza lingine lililofungwa na Olivier Giroud. Arsenal ilishinda 4-0.
Hata hivyo, katika dakika ya 79, Wenger alimtoa uwanjani ambapo alionekana kukasirika baada ya kuvua glavu zake na kuzipiga teke kuelekea kwenye benchi la timu yake, alipofika kwenye benchi akainama huku akiwa haangalii mchezo huo, kisha akajifunika na koti, lakini ndani ya uwanja alikuwa akiwabwatukia hovyo wachezaji wenzake kila walipokosea.
Tukio hili linafanana na lile ambalo alilifanya wakati wa mchezo dhidi ya Bournemouth wiki moja iliyopita ambao walitoka sare ya mabao 3-3.
“Wachezaji wote wamekuwa wakikasirika kila wakitolewa uwanjani, wengine wamekuwa wakionyesha wazi wengine wamekuwa wakificha, nipo kwenye soka kwa muda mrefu, hivyo najua.
“Nilipofanya maamuzi niliona nimefanya jambo sahihi kabisa, huyu ni mchezaji bora ambaye amekuwa akitaka kuona timu hii inashinda, hakika hakuna tatizo kati yangu naye,” alisema Wenger.
“Kila watu wana utamaduni wao. Amerika ya Kusini ni tofauti sana na Ulaya, Amerika ya Kaskazini ni tofauti na Ulaya Kaskazini, hivyo lazima umheshimu kila mtu kulingana na utamaduni wake.” .
Comments are closed.