The House of Favourite Newspapers

Wengi wanafeli kwa kupishana na waoaji, waolewaji!

0
Lovers in Hotel Room Preparing to Drink Wine --- Image by © Ragnar Schmuck/Corbis
Lovers in Hotel Room Preparing to Drink Wine — Image by © Ragnar Schmuck/Corbis

BILA shaka mpenzi msomaji ‘u-mzima’ wa afya na unaendelea na majukumu yako ya kila siku. Ni Jumamosi nyingine tunakutana katika uwanja wetu na kuweza kupata elimu ya uhusiano katika nyanja mbalimbali.

Kwa tuliokuwa pamoja, wiki iliyopita tulijifunza umuhimu wa kutambua kwamba mapenzi si kipato. Mapenzi si utajiri, kizazi cha sasa kinapotosha maana ya mapenzi. Watu wanatoa kipaumbele zaidi kwenye fedha kuliko utu wa mtu na moyo wenye mapenzi ya dhati.

Kutokana na kulevya na uchu wa fedha, wengi wameolewa na watu wasiowapenda na matokeo yake wameishia kwenye migogoro. Ndoa zao hazidumu, kila uchwao ni ugomvi kwa sababu ameolewa au kuoa mtu ambaye si sahihi. Alifuata fedha tu.

Leo tuiangalia mada nyingine nzuri yenye kichwa cha habari hapo juu. Marafiki, ujana una mambo mengi. Wengi wanaishi kwa mazoea. Kutokana na kasumba ya watu kuumizwa sana katika mapenzi, kila mmoja amekuwa mwepesi wa kukwepesha bawa lake na kuishi kwa tahadhari ya hali ya juu.

Mwanamke hata akutane na mwanaume wa aina gani, akamueleza sera nzuri kiasi gani, hawezi kumuelewa. Mwanaume atajitahidi kumueleza kwamba anamhitaji ili aweze kutulia naye, wajenge maisha lakini yeye wapi, hana muda wa kumchunguza wala nini.

Akilini anakuwa ameshajenga picha yake; kwamba hawa wote ndiyo walewale. Anaamua kujipa maisha ya uhuru, hataki kusumbuliwa. Anaamua kuwa mtu wa kutojali mapenzi. Hataki kuyumbishwa akili na mapenzi. Anaamua kuyachukulia poa.

Vivyo hivyo kwa wanaume, nao wanaamua kuyapotezea mapenzi. Wanaishi kwa kuigiza. Hawataki kusumbuliwa. Mwanaume anaamua tu kuwa na mtu lakini akili yake inakuwa haipo pale. Kama aliwahi kuumizwa na mwanamke mmoja, kila anayekutana naye mbele yake anasema ndiyo walewale.

Anaamua naye kuumiza wengine. Hana muda wa kumchunguza mwanamke, kujua ana upendo kiasi gani. Hajali kama ana nidhamu, amelelewa katika maadili, anafaa kuwa mke au la! Anatumia ujana wake kwa kubadili wanawake huku akiapa kutojipa ‘stress’ za mapenzi.

Mtu wa aina hiyo, akiambiwa na mpenzi wake kwamba anaomba waachane, anafurahia kweli. Moyoni anasema mbona umechelewa sana kufanya maamuzi. Kwake yeye lolote ni sawa tu. Uwepo usiwepo, haumuongezei wala kumpunguzia chochote.

Pasipo kujua, kila mmoja anakuwa anapishana na mwenzi sahihi. Maana mwanaume hana muda wa kumfanyia tathimini mwanamke na hata mwanamke naye hana muda wa kumchunguza mwanaume na kuona anafaa au hafai.

Ulimwengu mzima wa mapenzi unageuka kuwa wa watu wanaopishana na wenza sahihi. Kwa kupishana huko, kinachofuata baadaye huwa ni majuto. Maana hali hiyo ya kupishana inavyozidi kusonga mbele, umri nao unazidi kusonga.

Kuna muda unafika, mtu analazimisha kuingia kwenye ndoa maana umri unakuwa umemtupa mkono. Anashindwa kuelewa kwamba kama angefanya uchunguzi mzuri mapema, angekutana na mtu sahihi ambaye angeweza kujenga naye maisha. Matokeo yake anakuwa amechelewa. Yule aliyekuwa sahihi kwake, tayari anakuwa ameoana na mtu mwingine.

Kwa nini ukubali kupitwa na muda? Kwa  nini usimchunguze mtu mapema na kujua kama anafaa au la? Japo si kila anayekufuata atakuwa na nia ya dhati ya kuwa na wewe lakini hutakiwi kupuuza. Mke au mume mwema haji kama upepo.

Lazima ujipe muda mzuri wa kuwa karibu na mwenza aliyejitokeza, usiangalie uzuri au muonekano lakini umtathimini kwa kuangalia tabia zake, kuangalia historia yake na hata marafiki zake. Mshirikishe Mungu pia, muombe akuonesha kwamba huyo uliye naye ni sahihi?

Usiishi kwa kumkomoa mwenzako, usidharau hisia za mtu bali mtathimini huyo mtu ili uweze kujua kwamba anafaa au hafai. Kati ya watu wawili watatu ambao utawafanyia tathimini, kwa msaada wa Mungu utampata mwenza wa maisha.

Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply