Wenzako wanafanikiwa, wewe hakieleweki, wapi unakosea?
Hakuna anayeweza kuupinga ukweli kwamba, maisha ya sasa ni magumu, ugumu ambao kama mtu atabweteka na kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo upo uwezekano mkubwa wa kuingia katika mfumo wa maisha yasiyokuwa na mbele wala nyuma.
Lakini licha ya ukweli huo, bado nafasi zipo wazi kwa watu kuingia katika ulimwengu wa mafanikio. Hii itatokea tu kama mtu ataamua kupambana ipasavyo na kuhakikisha haingii katika kapu la umaskini ambalo limejaa wengi hata wasiostahili kuwemo.
Wapo watu na afya zao, nguvu za kutosha pamoja na maarifa waliyopewa na Mungu lakini bado wameridhika kuishi maisha ya kifukara huku wakitegemea misaada kutoka kwa watu wengine ili kuweza kusogeza siku.
Hakika hii ni hatari sana na uhatari huo unakuja hasa pale unapomuona mtu ambaye ana kila sababu ya kuwa miongoni mwa watu wenye mafanikio lakini yeye anaona hawezi kuwa hivyo huku akiwa na dhana kwamba, yeye ni miongoni mwa wale waliopangiwa kuishi maisha ya kifukara hadi mwisho wa maisha yao.
Wapo wanaoamini kwamba, Mungu kaleta ulimwenguni watu wa sampuli mbili. Yaani kuna maskini ambao hata wafanye nini hawawezi kuwa matajiri na kuna matajiri ambao wao wamepangiwa neema ëmwanzo mwishoí.
Watu wanaofikiria hivyo wapo huko mtaani na hakika wanakosea sana. Yaani wao wanaamini wameumbwa na umaskini na hawawezi kufanya chochote kitakachoweza kuwabadilisha kuwa miongoni mwa matajiri. Wenye dhana kama hizi ndiyo wale tunaowaona huko mtaani wakiishi maisha wasiyostahili kuishi.
Mtu kama ni kilema asiye na mikono wala miguu, anaweza kuwa sahihi akisema hana kitu anachoweza kukifanya akawa tajiri kutokana udhaifu aliokuwa nao lakini wewe ambaye una viungo kamili, nguvu pamoja na maarifa iweje uone uko sawa kuishi maisha duni?
Huoni kwamba utakuwa unajichoresha? Mimi nadhani ifike wakati ukae chini na ujiulize sababu za wewe kuendelea kuishi maisha mabaya wakati wenzako kila siku wanapiga hatua mbele.
Huenda kuna sehemu unakosea hivyo ni vyema ukaibaini na kufanya mabadiliko ya haraka ili na wewe uweze kuwa miongoni mwa wale waliotumia vizuri nafasi zao za kuletwa hapa ulimwenguni.
Kama unataka kutimiza wajibu wako wa kuletwa hapa ulimwenguni una kila sababu ya kufanya kazi kwa bidii bila kuridhika na hicho kidogo unachokipata sasa. Siku zote ota kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani bila kujali kwa sasa uko katika nafasi gani.
Ni hayo tu, tukutane tena wiki ijayo.