WEWE UKO DAR, YEYE ARUSHA, PENZI LA KWELI LITOKE WAPI?

MAPENZI yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu lakini mapenzi hayahaya yanafikia hatua ya kuwadatisha baadhi ya watu. Wengi wasiojua sarakasi zilizomo kwenye uwanja wa mapenzi wanashindwa kujua mchezo unakwendaje na kujikuta wakilizwa wasipate ile furaha waliyoitarajia.

 

Naamini tunajua usanii uliopo katika ulimwengu wa sasa wa mapenzi. Wengi wapo kwenye mapenzi ya kitapeli kwa kuingia kwenye uhusiano na watu ambao hawana mapenzi ya dhati bali wanatafuta pesa.

Kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya teknolojia, wapo ambao wamekuwa wakiingia kwenye uhusiano na watu ambao wako mbali. Unakuta msichana yupo Dar, anapata namba za simu za mvulana aliye Arusha na wanaanzisha uhusiano. Yawezekana kweli watu hawa wakaendeleza uhusiano wao na siku moja wakafunga ndoa na kuweka historia. Hata hivyo, baadhi wamejikuta wakiangukia kwa matapeli huku wakishea penzi na watu wengine bila kujua.

 

Nasema hivyo kutokana na ushuhuda wa mmoja wa wasomaji wa safu hii aliyejitambulisha kwa jina la Japhet ambaye alinieleza jinsi alivyofanyiwa usanii na binti ambaye alidhani amepata kumbe amepatikana. Hebu msikie uone jinsi mapenzi ya simu yalivyojaa ulaghai; “Nilionana naye mara moja mjini Arusha, tukapendana. Nikachukua namba yake na yeye akachukua yangu kisha mimi nikarudi Dar.

 

“Kuanzia hapo tukawa tunawasiliana, alikuwa akinipa maneno matamu sana huku akinionyesha kuwa kwenye moyo wake niko mimi tu. Nikawa najitutumua kwa matunzo, kila wiki lazima nimtumie pesa, vocha za hapa na pale, lengo langu aepukane na vishawishi vya wanaume wakware.

 

“Nilipoingiza suala la kutaka kwenda kwao ili akanitambulishe kwa wazazi wake hapo ndipo alipoanza kunichenga. Mara simu yake haipatikani, mara haipokelewi na nikituma meseji zikawa hazijibiwi. “Nikaanza kupata wasiwasi, nikalazimika kufunga safari hadi Arusha na nilipofika nikampigia simu, alipopokea na kumwambia niko Arusha akakata na kuanzia hapo sikumpata tena.”

 

Huyu ni mmoja tu kati ya wengi ambao waliyaamini mapenzi ya simu lakini mwisho wake yakawatokea puani. Hapa ni suala la kujiaminisha tu na huyo mtu wako ambaye mara nyingi mmekuwa mkiwasiliana kwenye simu. Unachotakiwa kujua ni kwamba, wapenzi wengi wa kwenye ni simu ni walaghai.

Watatumia maneno matamu kukulainisha lakini baadaye wanakugeuza kitega uchumi. Mizinga ya hapa na pale haitakosekana na meseji za ‘bebi sina credit’ kila siku lazima ziwepo, bado hujashtuka tu? Sikia msomaji wangu, sasa hivi wapo wasichana wa namna hii, anaingia kwenye uhusiano na wewe na kuonesha anakupenda sana lakini ukiacha wewe kuna wanaume wengine zaidi ya watatu.

 

Anachokifanya kila siku asubuhi anawatumia wote meseji kwamba ana shida ya pesa. Katika watatu hao hatakosekana mmoja au wawili ambao watatuma. Wapo wanaoendesha maisha yao kwa njia hiyo. Sasa kwa nini ukubali kuingia kwenye cheni ya wanaume kibao wanaomhudumia msichana mmoja ambaye anawachukulia nyie kama wajingawajinga wake?

 

Yes, nasema anawachukulia kama wajinga wake kwa kuwa ameweza kuziteka akili zenu na kuhisi mnapendwa kumbe hamna lolote, usanii mtupu! Nimelazimika kuiandika makala hii ili kujaribu kuwazibua masikio baadhi ya watu si, wanaume tu bali hata wanawake. Wapo ambao sasa hivi wako kwenye mapenzi ya kilaghai huku wakidanganywa na maneno matamu ya kwenye simu.

 

Ni muda muafaka kwako sasa kuutathimini uhusiano ulionao hasa kwa wewe ambaye uko mbali na mpenzi wako na kuangalia kweli anakupenda au anakulaghai na kukugeuza ATM huku akiwa na wengine? Usizubae katika hili. Hakika wajanja watakucheka

 

Loading...

Toa comment