The House of Favourite Newspapers

Wezi Watumia Mabomba ya Kinyesi Kuiba Mkwanja Benki

WEZI nchini Ubelgiji walilishangaza taifa hilo na ulimwengu baada ya kutumia mitaro na mabomba ya maji taka na kinyesi kusafiri hadi kwenye Tawi la Benki ya BNP Paribas Fortis, ambapo waliiba pesa zisizojulikana kiwango chake.

 

Wezi hao wanasemekana kutumia mabomba hayo ya upana wa sentimita 40 kupitia chini ya ardhi hadi eneo ambapo pesa zinahifadhiwa katika benki iliyo karibu na wilaya ya Antwerp Diamond Trading.

 

Polisi walifahamishwa kuhusu tukio hilo na walipofika eneo panapohifadhiwa pesa ndani ya benki hiyo, japo mlango ulikuwa umefungwa, masanduku 30 ya pesa yalikuwa yameibwa.

 

 

Hata hivyo, bado polisi hawajatangaza kiwango cha pesa ambacho wezi hao waliondoka nacho. Maofisa wanaosimamia maji na usafi wa mazingira mji huo, hata hivyo, walisema kuwa wezi hao walihatarisha maisha yao  kwa kutumia mbinu hiyo.

 

 

“Kwanza kabisa, kuchimba shimo ili kutokezea katika mabomba ya kusafirisha uchafu ilikuwa hatari kwani kulikuwa na uwezekano wa ardhi kuporomoka. Ndani ya mabomba hayo ya uchafu, kuna hatari nyingi kama hewa chafu inayotoka ndani ya uchafu huo,” alisema Els Liekens ofisa wa kampuni ya maji.

 

Wateja wa benki hiyo walighadhabishwa na hali ya benki kutowafahamisha kuhusu kisa chenyewe, wengine wakidai kuwa masanduku hayo yalikuwa yamehifadhi hazina zao za maisha.

 

 

“Watu wengi hawahifadhi pesa na vifaa vya utajiri pekee, bali pia vitu vya kifamilia,” alisema mmoja wao.

 

Wizi wa aina hiyo ambao ulitokea nchini Ufaransa mnamo mwaka 1976 uliwafanya wezi kuishi kwa miezi wakichimba ndani ya mabomba ya kusafirisha uchafu, kisha baadaye wakaiba mamilioni ya pesa pamoja na mali iliyokuwa ndani ya masanduku 200.

 

MASHIRIKA NA PETER MBURU

Comments are closed.