
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema dawa inayopulizwa mitaani katika baadhi ya nchi kama lengo la kuua virusi vya corona haisadiii chochote kwenye harakati za kupambana na janga hilo.
“Kupuliza dawa mtaani hakuui corona, inaweza kuleta hatari kwa watu kuugua magonjwa mengine yatokanayo na kuvuta hewa yenye kemikali,” limesema shirika hilo.
WHO wanakuja na tamko hili zikiwa zimepita takribani siku 25 tangu Rais Magufuli aliposema kuwa upulizaji wa dawa mitaani hauwezi kuua corona, ambapo alitoa kauli hiyo akiwa Chato mnamo Aprili 22, 2020.
“Huwezi kuua corona kwa kupuliza dawa kwenye mabasi na mitaani; ile unaua mende na wadudu wengine, ila hatujiulizi kwamba labda kupuliza ndiyo tunaongeza corona. Nimeona Dar es Salaam na Mwanza imepulizwa dawa tu na kasi ya wagonjwa imeongezeka Dar. Vyombo vya ulinzi chunguza nani alitoa hizo dawa. Hakuna virusi wanaokufa kwa ‘fumigation’; ni upuuzi,” alisema Magufuli.
Lakini pia rais wa WHO hivi karibuni amesema “Corona inaweza isiishe na inaweza ikazoeleka kama magonjwa mengine tu mfano ukimwi.”
Jambo hili ameshalisema Magufuli tangu Mei 3, 2020, akiwa Chato.
“Kama tunazuia hata kucheza mpira maana yake tunawaambia wapate #Corona. Najaribu kusubiri wataalamu wanishauri vizuri. Inawezekana tunaishi na huu ugonjwa kama watu wenye ukimwi, TB, surua na maisha yakaendelea. Tuache kuogopana na kutishana,” alisisitiza.

