Whozu: Staa wa Komedi Tangu Instagram Hadi Bongo Fleva

MWANZONI mwa miaka ya 2000 wakati watoto waliozaliwa miaka ya tisini wanakua, ilikuwa mara chache sana kukutana na wachekeshaji vijana wenye umri mdogo wanaofanya vizuri wakati huo ambapo wachekeshaji wenye umri mkubwa walikuwa wakipata nafasi zaidi.

Leo tupo kwenye Dunia ya Social Media, sehemu ambayo bila kuangalia umri, yeyote anayeweka nia ya kuitumia mitandao hii kikamilifu anapata nafasi ya kufanikiwa na kuionyesha jamii kile ambacho anakuwa nacho kwa ajili ya watu wake.

 

 

Whozu ni miongoni mwa mastaa ambao ni zao la mitandao ya kijamii aliyejipatia umaarufu kupitia Instagram kwa aina yake ya uchekeshaji na hatimaye sasa ni staa wa Bongo Fleva anayejitahidi kufanya kazi nzuri kwa ajili ya mashabiki wake. Safari yake huenda ikawa ndefu kuliko tunavyoweza kufikiria lakini kitu cha kujifunza hapa ni mafanikio yake kwa wakati huu ambapo tayari amefanikiwa kunga’aa kwenye nyimbo zaidi y 10 zikiwemo zake binafsi na zile alizoshirikishwa.

 

Aina yake ya uchekeshaji anayoitumia kwenye video za nyimbo zake na anazoshirikishwa zinatosha kueleza Whozu ana kipaji na amekuja wakati huu kwa makusudi ya Mungu kama vile ambavyo Whozu aliwahi kusema kwenye moja ya intavyuu zake.

Kwa muda ambao jamii ilianza kumuelewa kupitia nyimbo zake kama Tunawesha na Huendi Mbinguni, Whozu alipata bahati ya kuchaguliwa kuwa balozi wa kampeni za Uber na TCRA. Mbali na uimbaji, Whozu ni mwandishi wa nyimbo na moja kati ya nyimbo alizoandikia wasanii wengine ni “Kiki Ni Gigi’ wa Gigy Money.  Unaweza kuuona uwezo mwingine ambao msanii huyu amebarikiwa na amefanikiwa kuuonyesha.

 

Pongezi kwa wote waliomzunguka na kuhakikisha anazidi kusogea juu na kuwa chachu kwa vijana wa umri wake.   Hatua aliyofikia Whozu ni ile ya kujulikana kwa kila mtu hata asiyetumia Instagram hususani watoto na wazee. Whozu hahitaji kujitambulisha kwa mtu yeyote, anaishi ndoto zake na anaonekana kufurahia na kupenda anachokifanya, ndiyo maana yupo hapo tunapomuona na kumsikia leo.

Whozu ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wa karne hii wenye nguvu na ushawishi mkubwa kwa vijana wa umri wake. Yote yasingewezekana kama Whozu angetumia Instagram yake kutafuta ‘Wasichana Wazuri DM’, aliamua kuwa bidhaa na kujiuza kwa ‘followers’ wake waliompa thamani na kumfanya athubutu kufanya vitu vikubwa zaidi. Kuna namba kubwa ya wavulana wenye umri wa Whozu wanatumia Instagram kutafuta warembo wakati wengine wanatafuta mawasiliano na watu wanaowashawishi. Kama kijana unatumia Instagram kutengeneza namba ya ‘followers’ wasiokulipa na kutembelea DM za wasichana, jifunze kwa Whozu hutabaki kama ulivyo.

Tunamtakia kila la kheri. Tunapenda kumuona Whozu anakua siku hadi siku na hatimaye kuingia soko la kimataifa na kuendelea kuwashawishi vijana wenzake wanaomuangalia kama ‘role model’ kwa sasa.


Loading...

Toa comment