Wilaya ya Tanganyika Kuadhimisha Miaka 61 ya Uhuru kwa Kupanda Miti
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi,katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika Desemba 9 mwaka huu, jana Desemba 4 Halmashauri hiyo imezundua zoezi la kupanda miti ambapo jumla ya miche zaidi ya Milioni 3.5 ya matunda,mbao na ya kutunza mazingira inatarajiwa kupandwa msimu huu.
Akizindua zoezi hilo lililofanyika eneo la Mpanda kati kitongoji cha Mchakamchaka,Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema wameamua kufanya hivyo kama sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya uhifadhi wa mazingira.
Buswelu amesema kutokana na shughuli za kibinadamu yapo baadhi ya maeneo miti imepungua hivyo namna pekee ya kuirejesha ni kuhamasisha wananchi,taasisi na vyama vya msingi pamoja na AMCOS wanashiriki zoezi hilo.
Mwenyekiti wa chama cha msingi Mpanda kati AMCOS Philbert Ngula amesema malengo waliyojiwekea ni kila mwanachama wa AMCOS kupanda miti 200 na kupitia mashamba ya pamoja ya AMCOS zaidi ya miti 3700 inatarajiwa kupandwa huku kila mwananchi akitakiwa kupanda walau miti hamsini.
Mwakikishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Ambwene Yona ambaye ni mkuu wa kitengo cha mawasiliano amesema mkakati mwingine ni kika taasisi ya Umma kupanda miti isiyopungua 1000 hiyo ikiwa ni kuhakikisha Tanganyika inabaki ya kijani.
Kwa upande wake afisa ushirika wa halmashauri ya Tanganyika Jaliwa Amani ametoa wito kwa wakukima wa tumbaku kuungana kwa pamoja katika zoezi hilo kwa kuwa wao ndio watumiaji wakubwa wa miti hasa wakati wa uchomaji wa tumbaku.