The House of Favourite Newspapers

Will Smith Hatarini Kupokonywa Tuzo Ya Oscar

0


Licha ya kuomba msamaha kwa waandaaji wa Tuzo za Oscar kwa tukio alilolifanya la kumzaba kibao mshehereshaji namchekeshaji maarufu, Chris Rock, mwigizaji mkubwa wa filamu za Hollywood, Will Smith yupo kwenye hatari ya kunyang’anywa tuzo aliyoshinda.

Smith alitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo za Oscars katika kipengele cha mwigizaji bora wa mwaka, kupitia filamu ya King Richard ambayo ameigiza kama Richard Williams, baba wa nyota wa mchezo wa tenisi duniani, Venus na Serena Williams, ikiwa ni mara yake ya kwanza kupata tuzo hiyo kubwa duniani.

Tukio la kumzaba kofi Rock, ambalo lilinaswa na kurushwa mubashara duniani kote kutokea katika Ukumbi wa Dolby Theatre, Hollywood nchini Marekani, limewakasirisha waandaaji wa tuzo hizo ambapo inaelezwa kwamba mjadala mkali umefanyika kumjadili Smith kama anastahili kuendelea kubaki na tuzo hiyo.

Baada ya kukabidhiwa tuzo yake, Will Smith aliutumia muda wa kutoa salamu za shukrani, kuwaomba radhi wote waliokasirishwa na kitendo cha kumpiga kibao Rock akiwa jukwaani na kueleza kwamba lilikuwa ni tukio ambalo haliwezi kusameheka kwa urahisi.

Sababu kubwa iliyomkasirisha Will Smith mpaka akafikia hatua ya kufanya tukio hilo ambalo halikutarajiwa, ni baada ya mshereheshaji huyo ambaye pia ni mchekeshaji, kumtania mke wa Will Smith, Jada Pinkett Smith kuhusu mtindo wake wa kunyoa nywele zote kichwani.

Rock alisikika akisema anampenda Jada huku akisema anaisubiri sehemu ya 2 ya filamu ya G.I. Jane, mzaha ambao haukuwafurahisha Smith na mkewe. Katika kuweka kumbukumbu sawa, G.I. Jane ni filamu ya mwaka 1997 iliyomuonesha mwigizaji Demi Moore akiwa amenyoa nywele zote kichwani na kubaki na upara.

Baada ya kukasirishwa na utani huo, kama masihara Smith alisimama na kuanza kutembea kuelekea jukwaa kuu alipokuwa amesimama Rock akiendelea na mizaha yake.

Hakuna aliyeelewa mara moja nini kinachokwenda kutokea, watu wakawa wanaendelea kucheka kutokana na maneno aliyokuwa akiendelea kuyatoa Rock kumhusu Jada na muda mfupi baadaye, Will Smith akawa ameshamsogelea Rock mwilini.

Kufumba na kufumbua, alimzaba kofi la nguvu Rock na kusababisha watu wote wapigwe na butwaa, Rock naye akapigwa na bumbuwazi kwa sababu hakuwa ametegemea tukio kama hilo, akajishika shavu alilopigwa kofi huku akibadilisha mazungumzo.

Will Smith alirudi kwenye sehemu yake na kukaa lakini katika hali iliyowafanya wote wajue kwamba kumbe alikuwa amekasirika kisawasawa, alianza kumrushia maneno makali mshereheshaji huyo na kumwambia hataki aendelee kumtajataja mkewe bila sababu.

Licha ya kuomba msamaha jukwaani kwa tukio hilo lisilo la kiungwana, Will Smith pia aliitumia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Instagram kuendelea kuomba radhi, safari hii akimuomba pia radhi Rock kwa kitendo alichomfanyia.

“Vurugu katika namna yake yoyote ni sumu na hubomoa. Tabia yangu usiku uliopita katika tukio la utoaji wa tuzo haikubaliki na haisameheki. Utani kuhusu mimi ni sehemu ya kazi yangu lakini utani kuhusu ugonjwa wa mke wangu ulivuka mipaka na kunifanya nishindwe kudhibiti hisia zangu.

“Napenda kuomba radhi hadharani kwako Chris. Nilitoka nje ya mstari na nilikosea. Najisikia vibaya kwamba tukio hilo limeenda tofauti na mipango ya jinsi ninavyotaka kuwa. Hakuna nafasi ya vurugu katika dunia iliyojawa upendo na huruma,” aliandika Smith.

Pia aliomba radhi kwa mara nyingine kwa waandaaji wa tuzo hizo na familia ya Williams ambayo kupitia filamu waliyoitengeneza kuhusu maisha yao, ndiyo Smith aliyopatia tuzo.

Bado Rock hajajibu chochote kuhusu msamaha huo wala hajatoa maoni yoyote lakini wanaharakati mbalimbali wanaendelea kupaza sauti wakitaka staa huyo anyang’anywe tuzo hiyo kwa kuonesha tabia mbovu hadharani, tena huku akijua kwamba tukio hilo lilikuwa likirushwa ‘live’ na runinga duniani kote.

 

Leave A Reply