WINGA msumbufu wa TP Mazembe, Phillipe Kinzumbi ameweka wazi kuwa ameamua kukubali kumwaga wino Yanga kutokana na mambo matatu makubwa ambayo yamemvutia ndani ya timu hiyo.
Nyota huyo usajili wake unatajwa kumalizwa na vigogo wa Yanga ambao walienda nchini DR Congo kwenye mechi ya marudiano kati ya Yanga na TP Mazembe ambayo ilipigwa Uwanja wa Mazembe, jana Jumapili.
Kinzumbi anakumbukwa kutokana na kuwasumbua mabeki wa pembeni wa Yanga, Djuma Shaban na Lomalisa Mutambala kwenye mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, na Yanga wakashinda mabao 3-1.
Winga huyo ameliambia Championi Jumatatu, kuwa amekubali kujiunga na timu hiyo kutokana na mambo matatu ambayo ni ukubwa wa Yanga kwa sasa, hatua ambayo imepiga soka la Tanzania na kuwa na marafiki wengi ndani ya timu hiyo akiwemo Djuma, Yannick Bangala na Lomalisa.
“Kwa sasa ndani ya ligi ya DR Congo hakuna nyota ambaye atakataa kutua Yanga kutokana na ukubwa wao kwa sasa sambamba na malengo yao kwa ujumla, pia mpira wa Tanzania kwa sasa upo juu, mchezaji akicheza Tanzania kwa sasa basi anapata vitu vingi sana vya tofauti ambavyo havipo katika ligi zetu na pia nina marafiki wengi ndani ya timu hiyo,” anasema Kinzumbi.
Stori na Macro Mzumbe