Wizara ya Afya yamvaa Faiza

Faiza Ally.

Dunia ina mambo! Kila kukicha kwenye ulimwengu huu wa mitandao ya kijamii kunazuka jambo jipya ambapo siku chache zilipita, msanii wa filamu za Kibongo, Faiza Ally ametengeneza vichwa vya habari baada ya kutupia picha ya utupu akiwa anajifungua.

Picha hiyo inayomuonesha akiwa mtupu ndani ya chumba cha kujifungulia ‘leba’ huku akiwa amepakata kichanga chake, imezua gumzo la aina yake huku watu kibao wakimtukana na kumlaumu kuwa kitendo hicho walichodai kinawadhalilisha wanawake.

 

“Yaani hawa watu wanaiga mambo ya akina Kim Kardashian halafu wanayaleta huku Tanzania wakati siyo utamaduni wetu, hii kweli siyo sawa na anawadhalilisha sana wanawake maana kujifungua ni jambo linalohitaji faragha kubwa, lakini yeye ameanika picha,” alisema mdau mmoja kwenye mtandao wa Instagram.

Licha ya watu wa kawaida kumponda Faiza kwa kitendo chake hicho, pia mastaa kibao nao walimjia juu kama moto wa kifuu kwa ujinga huo, wasani hao ni pamoja na Batuli, Riyama, Chuchu Hans, Odama, Isabela Mpanda, Lulu Diva Sandra na wengine kadhaa.

 

Mastaa hao walisema kitendo cha msanii mwenzao huyo ni udhalilishaji na kinamshushia hadhi kwenye jamii japo inawezekana pia inachangiwa na malezi aliyolelewa.

“Huo siyo ujanja hata kidogo na wala siyo uzungu, sisi ni Watanzania, tuna maadili yetu ambayo huwezi kuyachanganya na Ulaya, tunaweza kumlaumu lakini pengine tatizo ni la malezi,” alisema Sandra.

Risasi Mchanganyiko lilipotaka kupata maoni ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, lilifanya mawasiliano na waziri wake, Ummy Mwalimu, lakini kwa muda wote simu yake iliita bila kupokelewa.

 

Hata hivyo, msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema ni jambo la kusikitisha kwa vile maadili ya kitanzania hayaruhusu hilo suala, lakini pia wao kama wizara hawajapendezwa na hawaruhusu picha kama hizo kupigwa.

“Lakini kwa kuwa aliweka katika mtandao wa kijamii, ni suala la watu wa sheria za mtandao kuona ni namna gani wanaweza wakadhibiti jambo hili ambalo ni baya na lisilofaa kabisa,” alisema Mwamwaja.

 

FAIZA ANASEMAJE?

Alipotafutwa Faiza ili kueleza kilichosababisha kuanika picha hiyo alisema alifanya hivyo kwa kuwa alijisikia raha na anajivunia kuwa mama kwani wapo wanaotamani kuwa na watoto lakini hawapati.

“Yaani hiyo picha mbona jambo la kawaida sana wala siyo ‘big deal’ kama watu wanavyozungumzia? Kila mtu amezaliwa kuanzia mabibi zetu na mababu sema tu hawakupiga picha, kuhusu kuchukuliwa hatua sitajuta kwani ndiyo nitajifunza ila nilifanya hivyo kwa kuwa najivunia kuingia leba kwa kweli,” alisema Faiza.

 

Wakati gazeti hili likienda mitamboni, habari zilizotolewa na mwanamke huyo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Instagram, alisema vyombo vya usalama vimechukua simu yake kwa ajili ya uchunguzi ambao haelewi utachukua muda gani.

Imeandikwa na Mayasa Mariwata na Gladness Mallya | RISASI MCHANGANYIKO.

 

GLOBAL HABARI: KUBENEA ASEMA HAYUPO TAYARI KUACHIA UBUNGE WAKE

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment