The House of Favourite Newspapers

Wizara Ya Afya Yatoa Tathimini Kuhusu Ugonjwa Wa Kipindupindu

0

Kigwangalla (1) Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangala (kushoto) akisoma ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari.

Kigwangalla (2)Kigwangala (katikati) akisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabari (hawapo pichani) pembeni yake ni baadhi ya viongozi wa wizara yake.

Kigwangalla (3)Mkutano ukiendelea.

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Naibu Waziri wake, Dk. Hamis Kigwangala, leo imetoa tathimini kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu ambao umekuwa ukiisumbua Tanzania tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na wanahabari leo katika ofisi za wizara hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam, Kingwangala alisema katika kipindi cha wiki iliyoanza Januari 4 hadi 10, mwaka huu, kumekuwa na jumla ya wagonjwa 615 walioripotiwa nchini huku vifo vikiwa ni vitatu .

Amesema mikoa ambayo imeripotiwa kuwa na ugonjwa huo ndani ya wiki moja iliyopita sasa imepungua kutoka 21 na kufikia 11 ambayo ni Morogoro, Arusha, Singida Manyara, Pwani, Dodoma, Geita, Mara,Tanga, Mwanza na Simiyu.

Alisema katika mikoa hiyo, Mkoa wa Morogoro ndiyo unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi ambao ni 87 kutoka Manispaa ya Morogoro na 66 katika Halmashauri ya Morogoro, huku akiutaja Mkoa wa Arusha kushika namba mbili kwa kuwa na wagonjwa 50.

Aidha Kigwangala alisema mikoa iliyokuwa na maambukizi hayo na wiki iliyopita haikuripotiwa ni Mbeya, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Lindi na Dar es Salaam ambako ndipo ugonjwa ulipoanzia, miezi minne iliyopita.

Hata hivyo, Kigwangala amezitaka mamlaka za mikoa na halmashauri pamoja na watendaji wake kote nchini kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko wa ugonjwa huo hatari pamoja na kuchukua hatua stahiki za tahadhari kwa kusimamia utekelezaji wa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unapatikana ikiwa ni pamoja na uwekaji wa dawa ya krolini na kupima usalama wa miji mara kwa mara.

Pia upatikanaji wa vyoo bora katika kila kaya, kuelimisha kina baba lishe na mama lishe kuhusu kanuni za afya na kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini.

Tathimini zinaonesha kuwa, tangu kuanza kwa ugonjwa huo Agosti, mwaka jana, jumla ya watu 13,491 wameripotiwa kuugua ugomjwa huo huku watu 205 wakiripotiwa kufariki dunia.

NA DENIS MTIMA/GPL

Leave A Reply