Wizara ya Maji na Kilimo Kushirikiana Miradi ya Maji na Umwagiliaji Ziwa Victoria na Tanganyika
Viongozi wawili wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji wamekutana leo tarehe 4 Septemba 2024 jijini Dodoma na kuahidi kushirikiana pamoja katika miradi ya maji na umwagiliaji ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara hizo.
Viongozi hao, Mhe. Jumaa H. Aweso (Mb), Waziri wa Maji na Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo wamejadiliana mikakati mbalimbali ya awali ya kukutanisha wataalamu wa pande zote mbili ili kuanza kushirikiana katika miradi ya Ziwa Victoria ambao umeshaanza kufanyiwa kazi kwa ajili ya kusafirisha maji hadi Mkoa wa Dodoma; na Ziwa Tanganyika ambao umelengwa kuhudumia Mikoa ya Ruvuma, Kagera, Kigoma na mingine.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Mhandisi Mwajuma Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Dkt. Hussein Omar, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Raymond Mndolwa, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Mhandisi Anna Mwangamilo, Mkurugenzi wa Idara ya Zana za Kilimo katika Wizara ya Kilimo.
Kwa upande wa Wizara ya Kilimo, jukumu lake ni kuhakikisha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) inakuwa sehemu ya timu ya wataalamu wa Wizara ya Maji katika kuhuisha kazi za skimu za umwagiliaji katika maeneo ya miradi hiyo ili wakulima waweze kunufaika katika shughuli za Kilimo cha umwagiliaji. Miradi hiyo ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika ina malengo ya kuwa na huduma ya maji kwa matumizi ya binadamu, maji ya matumizi ya wanyama na maju ya matumizi ya kilimo cha umwagiliaji.
Aidha, timu za wataalamu kutoka Wizara hizo zimepanga kukutana tena mwezi huu ili kujipanga zaidi, ikiwa ni pamoja na kutembelea miradi inayofanana na hii nchini China kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi kwa manufaa mapana ya Taifa katika sekta za uzalisha ni nchini.