Wizi wa kura!

MIZENGWENa Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutuhumiwa kupitia gazeti moja linalotoka mara moja kwa wiki (siyo Uwazi Mizengwe) kusajili vijana wapatao 265 kwa ajili ya zoezi la kuiba kura katika uchaguzi mkuu ujao, mambo mapya yameibuka, gazeti hili linaripoti.

ILIVYOKUWA

Gazeti hilo lilinukuu vyanzo vyake vikisema kuwa vijana hao ambao wamebatizwa jina la makapteni, waliopatiwa mafunzo ya siku mbili kisiwani Zanzibar, miongoni mwa kazi watakazopewa, ni kuwapa mafunzo wenzao wengine wapatao 60,000 ambao watasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kufanikisha ushindi kwa chama hicho tawala.

Likaendelea kueleza kwamba vijana hao waliosajiliwa, kazi yao nyingine itakuwa ni kuwatafuta na kuwashawishi watu maarufu, viongozi wa dini na wasanii ili wafanye kazi ya kuwahamasisha watu kuiunga mkono CCM, ikiwa pia ni pamoja na kutumika wakati wa uchaguzi, hasa pale itakapohitajika kuhamisha masanduku ya kura.

Kwamba gazeti hilo liliunasa waraka wa siri wa chama tawala wenye kurasa 39, umeonesha makapteni hao watalipwa kiasi cha shilingi 125,000 kwa wiki zikiwa ni posho na matumizi ya simu.

WATUHUMIWA NI AKINA NANI?

Gazeti hilo liliwataja kwa majina, majimbo waliyopewa na kuanika namba za simu za vijana hao 265, wakidaiwa kutumiwa na waratibu wa ushindi wa uchaguzi kwa chama hicho ambacho kimeunda serikali za awamu zote tangu uhuru.

Mpango wa mbinu hizo chafu unadaiwa kufanywa baada ya kuona CCM ipo katika wakati mgumu, kufuatia mafuriko ya watu katika mikutano ya kampeni inayohutubiwa na mgombea wa urais wa Chadema, anayeungwa mkono na vyama vilivyo chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Ngoyai Lowassa.

“Hawa watu ni muhimu kuwajua na kuwafuatilia kwa sababu ndiyo watahusika katika mikakati ya wizi wa kura, pale itakapobidi hasa kwenye kuhamisha masanduku ya kura,” liliripoti gazeti hilo juu ya sakata hilo.

WATUHUMIWA WANASEMAJE?

Kufuatia madai hayo mazito, Uwazi Mizengwe liliwatafuta baadhi ya watuhumiwa waliotajwa na kufanikiwa kuongea nao juu ya suala hilo.

Jimson Sigala, aliyetajwa katika orodha hiyo akiwa nafasi ya nane, anayetajwa kupewa kazi hiyo katika Jimbo la Mufindi Kusini, alipatikana kupitia namba ya simu iliyowekwa katika gazeti hilo na alipoulizwa kama ndiye mwenye jina hilo alikiri ni yeye.

“Ndiyo, hilo ni jina langu.”

“Wewe unaishi Mufindi Kusini?”

“Ndiyo.”

“Kuna habari katika gazeti, jina lako linatajwa kama miongoni mwa vijana 265 waliopewa mafunzo maalum na CCM kwa ajili ya wizi wa kura wakati wa uchaguzi mkuu, unaweza kutoa ufafanuzi juu ya hili?”

“Mimi sijaliona hilo gazeti kwa hiyo sijui kilichoandikwa lakini kama ni mafunzo, ni kweli. Mimi ni Katibu Mwenezi wa CCM, Kata ya Mtwango, nilipewa mafunzo ya jinsi ya kueneza siasa za chama katika eneo langu. Eti nimefundishwa kuiba kura? Hivi ndugu mwandishi, nitawezaje kuiba kura wakati katika vituo kila chama kina wakala wake?”

Alipoulizwa kama anamfahamu Asumta Ntende, ambaye ametajwa juu yake kama kijana mwingine aliyepewa kazi katika jimbo hilo, lakini simu yake haikupatikana, alikiri kumfahamu na kusema kuwa naye ni kiongozi kwani ni katibu wa mbunge wa jimbo hilo.

Magreth Obedi ambaye ametajwa kupewa kazi katika Jimbo la Manyoni Magharibi, naye alikiri jina na eneo alilopo ikiwa ni pamoja na kushiriki kozi hiyo, lakini aliposomewa tuhuma zake alisema:

“Mimi hata sielewi unachoniambia, mimi ndiyo kwanza nimetimiza miaka 18, nilipelekwa katika mafunzo kama mwanachama, sikupewa maelekezo yoyote zaidi ya kutakiwa kuwahamasisha vijana wenzangu kukipigia kura chama chetu.”

Mwingine aliyefikiwa na gazeti hili, ni mtu aliyetajwa kwa jina la Vicent Mathayo wa Karatu, ambaye alisema yeye ni mzaliwa na mkazi wa Karatu na kwamba ni mwana- CCM hai.

Kuhusu tuhuma za kushiriki mafunzo ya kuiba kura katika uchaguzi mkuu, mtu huyo alikuja juu huku akionekana kumtisha mwandishi, akijitaja kwamba yeye ni Mkuu wa Wilaya (hakutaja kituo chake cha kazi) hivyo hatakiwi kuulizwa maswali ya kijinga na kipumbavu. Mtuhumiwa mwingine, Michel Amin wa Hai mkoani Kilimanjaro, alipopatikana na kusomewa mashtaka yake, aliomba apigiwe baadaye ili atoe ufafanuzi kwani wakati huo alikuwa akifanya kazi f’lani.

NAPE AFAFANUA

Uwazi Mizengwe lilimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ili atoe ufafanuzi wa tuhuma hizo alizoambiwa ni nzito na kubwa kwa chama chake.

“Hizo siyo tuhuma nzito wala kubwa hata kidogo, ni tuhuma za kijinga za kila siku ili kuhalalisha kushindwa kwao. Hatujawahi kuwafundisha watu kuiba kura, ila hizo ni mbinu zao kuwahadaa wafuasi wao ili wakishindwa katika sanduku la kura, waamini kuwa wameibiwa.

“Ni watu wa ajabu sana Ukawa, sisi mgombea wetu anatumia dakika 40-45 jukwaani kujinadi na kuomba kura kwa wananchi, wao mgombea wao anatumia dakika mbili hadi tatu, sasa watu watakuelewa vipi sera zako? Kwa kuwa wameona hawawezi kuwashawishi watu, wanatengeneza mazingira ya kuhalalisha kushindwa kwao kwa kisingizio cha kuibiwa kura,” alisema Nape.

Alipoulizwa juu ya ukweli wa kuwepo kwa mafunzo hayo ya vijana, Nape alikiri kuwa ni kweli wamekuwa na mafunzo kwa makada wao, lakini siyo kwa ajili ya kuiba kura, bali kwa kuwaelekeza mambo mbalimbali yanayohusu chama chao.

“Semina na kozi za chama zimekuwepo tokea enzi za Mwalimu Nyerere, tunawapa mafunzo makada wetu mara kwa mara, tunazo kozi za Wenyeviti wa Mikoa, Wenyeviti wa Wilaya,

Makatibu Waenezi na makundi mbalimbali ya wanachama wetu, leo mtu anakuja anasema ni kwa ajili ya wizi wa kura, hizo ni propaganda, kama nilivyokuambia, wameshajua hawana chao, wanatafuta pa kufia.

“Hivi kama sisi tuna uwezo wa kuiba kura, unadhani hatuipendi Pemba sisi, kwa nini hatupati ushindi wa Moshi Mjini, Arusha

je, unadhani hatuitaki Karatu sisi? Kama tungekuwa na uwezo huo, nafikiri haya maeneo yanayotusumbua kila mara, tungetumia mbinu hizo kuiba kura,” alisema katibu huyo.

Mara kwa mara, viongozi wa Ukawa wamekuwa wakilalamika juu ya mipango ya kuiba kura inayotajwa kufanywa na CCM na wakati mwingine wamekuwa wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa inashirikiana na chama tawala kucheza rafu katika maeneo mbalimbali, tuhuma ambazo hata hivyo, imekuwa ikikanusha mara kwa mara.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS

globalbreakingnews.JPG
Toa comment