The House of Favourite Newspapers

WIZI WA LAPTOP UDSM, MREMBO HUYU AWATESA ASKARI

0
Maisara baada ya kudakwa.

MREMBO  mmoja jijini, aliyefahamika kwa jina moja la Maisara anawatesa polisi kuhusiana na wizi wa Kompyuta mpakato (Laptop) unaoendelea katika mabweni mbalimbali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya mlimani.

Mwanadada huyo alikamatwa Agosti Mosi, mwaka huu katika bweni namba moja (HALL 1) akiwa ameiba laptop tatu za wanafunzi wa chuo hicho, kitu ambacho kinadaiwa kuwa ni kawaida yake, kwani miezi michache nyuma, anadaiwa kufanya kitendo kama hicho katika bweni namba saba chuoni hapo.

Risasi Jumamosi lilifika Chuo Kikuu na kuzungumza na mmoja wa viongozi wa mabweni yaliyotajwa baada ya kuonyeshwa picha, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akisema yeye hakuwa na mamlaka ya kuzungumzia suala hilo na kulielekeza gazeti hili kumtafuta Ofisa Uhusiano wa Chuo.

Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jackson Isdori alisema anazo taarifa za kutokea kwa tukio hilo, lakini chuo kama taasisi, hakihusiki na wizi unaowahusu wanafunzi, kwani ni jukumu lao kufuatilia wenyewe kwa mamlaka zinazohusika.

“Ni juu ya mwanafunzi aliyeibiwa kufuatilia mali zake polisi au hata mahakamani. kama mali zilizoibwa ni za chuo, hapo ndipo tungekuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Muliro Jumanne Muliro.

Katika Kituo cha Polisi Chuo Kikuu, maofisa waliokutwa hapo licha ya kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, walikataa kulizungumzia kwa madai kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Muliro Jumanne Muliro ndiye mwenye jukumu hilo.

Afande Muliro alipotafutwa na kuelezwa juu ya tukio hilo, aliomba muda ili ‘a-cross check’ na baada ya muda mchache alipiga simu chumba cha habari na kufunguka ifuatavyo; “Ni kweli hilo tukio limetokea na siyo mara ya kwanza.

Huyo mtuhumiwa anafahamika kwa jina moja tu la Maisara na amekuwa akifanya matukio hayo mara kwa mara. Polisi ikimkamata, wanafunzi walioibiwa huomba kurejeshewa tu vitu vyao, lakini tukiwaambia waje mahakamani kutoa ushahidi, wanakubali lakini siku ya kesi hawaonekani.

“Hii ndiyo sababu ikifika wakati mtuhumiwa anapelekwa mahakamani bila shahidi kufika, anaachiliwa na hivyo anarudia tena mchezo wake. Hakimu hawezi kumhukumu mtuhumiwa bila kujiridhisha. “Jamii ya wanafunzi wa Chuo Kikuu wanapaswa kutambua kuwa tatizo hili haliwezi kwisha bila wao kujitokeza mahakamani na kutoa ushahidi juu ya tabia hii.”

NA: WAANDISHI WETU| RISASI| DAR ES SALAAM

Leave A Reply