WOLPER AJUTA KUMPA PENZI HARMONIZE

AMA kweli mwanzo wa penzi ni mtamu kama asali, lakini mwisho huwa ni shubiri! Hivyo ndivyo hali ilivyo kati ya wapenzi zilipendwa, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’na Jacqueline Wolper Massawe, Risasi Jumamosi limesheheni ubuyu kamili. 

 

Wolper ambaye ni staa wa filamu za Kibongo na mbunifu wa mavazi, yupo kwenye majuto mazito akijiuliza: “Hivi kwa nini nilimpa Raj (Harmonize) penzi langu?”

 

HAKUSTAHILI

Wolper anaamini moyoni mwake kuwa Harmonize kutoka kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) hakustahili kufaidi penzi lake. Wolper ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro anayeaminika kuwa na hasira kali, alifikia hatua ya kulieleza gazeti hili hayo baada ya mpenzi wake huyo wa zamani kutupia picha yake na mpenzi wake wa sasa, Sarah kwenye ukurasa wake wa Instagram, wakiwa katika mavazi ya kuogelea kisha kuwauliza mashabiki ni nani alinoga kwenye video za nyimbo zake?

MATUSI

Kwa mujibu wa Wolper, kitendo hicho kilisababisha ashushiwe matusi ya nguoni, jambo ambalo limemfanya ajipange kumfikisha Harmonize mahakamani kwa kumchafulia jina. Katika mahojiano na Risasi Jumamosi, Wolper alionesha kukerwa na kitendo hicho ambapo mahojiano yalikuwa hivi;

 

HUYU HAPA WOLPER

Risasi Jumamosi: Harmonize alivyoposti picha yako akikulinganisha na Sarah, ni jambo ambalo unalifahamu au kuna ugomvi wa chinichini unaendelea kati yako na yeye?

Wolper: Dah! Kwanza mimi kuwa na ugomvi na mtu mdogo kama Harmonize ni kujishusha sana. Mimi unaweza kunikuta kwenye ugomvi na mfanyabishara mwenzangu, tena labda awe amenidhulumu kontena langu, chini ya hapo sina tatizo na mtu yeyote yule.

Risasi Jumamosi: Sasa kwa nini amefanya vile kukulinganisha na Sarah?

Wolper: Kwanza kabisa mimi namshangaa sana mwanamke ambaye yuko naye, mwanaume wake anaposti vipi picha ya mwanamke wake wa zamani naye anakaa kimya? Maana kufanya vile ni kwamba bado mwanaume wake anamkumbuka yule mwanamke wa zamani ndiyo maana anamfuatafuata.

 

Risasi Jumamosi: Kwa hiyo hukumpigia hata simu kumuuliza?

Wolper: Yaani kumbe hunielewi? Mimi siyo wa levo ya Raj (Harmonize), yaani mpaka niinue simu kumpigia, maana mimi ndiye nilimfanya awe na jina baada ya kutoka kijijini kwao na ushamba wake, moja kwa moja akapata nafasi ya kuwa na mimi kimapenzi. Hujui kama siyo rahisi na ndiyo maana anahangaika kwa sababau ameshanimisi.

Risasi Jumamosi: Sasa baada ya kuona ameposti vile umechukua hatua gani?

Wolper: Nilijipanga kumshtaki maana amenikosea na angenilipa fedha nyingi tu, lakini kwa vile familia yangu inamcha Mungu tumeacha kama ilivyo.

Risasi Jumamosi: Siyo kwamba amekushirikisha jambo hili na kwamba ni kiki ya wimbo wake mpya?

 

Wolper: Hapana…huko mimi nilishapita, yeye alinitumia mimi kama ngazi ya kumfikisha huko juu, sasa asinitumie tena kumpandisha, aniache, maana hata alivyoweka hivyo ningeweza kuongea au hata kwenda kwenye mahojiano mbalimbali, lakini nimemdharau.

Risasi Jumamosi: Haya asante sana kwa ushirikiano wako.

Wolper: Asante sana.

Baada ya kuzungumza na Wolper, gazeti hili lilimtafuta Harmonize na baada ya kumpata, kabla hata ya kumsomea maelezo alimwambia mwandishi kuwa atampigia na hakupiga tena wala kupokea simu kila alipopigiwa kwa siku nzima.

 

TULIKOTOKA

Wakati wakiwa wapenzi yapata mwaka mmoja uliopita, Harmonize alimtumia Wolper kama video queen kwenye wimbo wake wa Niambie na safari hii akamtumia Sarah kwenye wimbo wake mwingine wa Niteke ndiyo chanzo cha yote yaliyojiri

STORI: Imelda Mtema,Risasi Jumamosi


Loading...

Toa comment