The House of Favourite Newspapers

Wolper, Punguza Ushamba Basi!

0
Jacqueline Walper ‘Wolper Gambe’

 

NINA kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na fadhila zake kwangu, lakini nisiwe mchoyo kumshukuru kwa niaba yako wewe msomaji wangu, hasa kwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa safu hii ya Barua Nzito. Leo nimeona itapendeza zaidi nikiwasiliana na dada yangu Jacqueline Walper ‘Wolper Gambe’ ambaye kwa sasa yuko na shemela yetu, a.k.a Kibenteni chake, Brown.

 

Siku zote nimekuwa nikimheshimu sana Wolper, maana ni mmoja kati ya wadada wanaojua nini wanafanya kwenye kazi yake. Sijawahi kugombana naye kwa ishu yoyote ile na mara nyingi tumekuwa tukifanya kazi kwa ushirikiano mzuri.

 

Licha ya ukongwe wake katika filamu, lakini pia kwa kumuangalia, ni mtu mzima sasa, ambaye hata hivyo, suala la mapenzi linaonekana kumtesa bado, maana hajatulia. Leo atakuwa na mtu anayeitwa Mkongo, kesho tunasikia anajirusha na staa mwenzake wa muziki, mara ndiyo kama hivi, yupo na bwana mdogo
mmoja hivi sasa.

Huenda hili lina mchango mkubwa katika kumpa kile ambacho wenyewe wanasema ‘stress’ maana kuna mambo ya kiutu uzima anayefanya ambayo si rahisi kuamini kuwa yanatoka kwake, hasa kutokana na heshima ambayo tayari amejiwekea kwa jamii. Katika ukurasa wake wa Instagram mwishoni mwa wiki iliyopita, Wolper alitupia video fupi ikimuonyesha akiwa amelala kitandani chumbani, huku amejifunika shuka na mpenzi wake wa sasa, Brown akiwa ndiye anayepiga picha hiyo.

 

Ni kama wapenzi waliokuwa wanajiandaa kulala au wametoka kulala! Mambo ya ujana nayo wakati mwingine yanaweza kumfanya mtu akasahau thamani yake mbele ya jamii au hata kufikiri kuhusu wazazi na ndugu wengine wanaomheshimu, ambao wanaweza kuwa na maswali mengi yanayokosa majibu kwa kuziona picha zake hizo. Jamani dada, mambo ya chumbani si yanabakia kuwa hukohuko na siyo kujiachia hovyohovyo?

 

Faragha ina heshima yake na ina mahala pake siyo kupiga picha na kujiwekea tu hovyo kwenye mitandao ya kijamii. Sijui una maana gani dada, unatafuta kiki au unajaribu kumuumiza roho bwana’ako wa zamani ajue kuwa una kitu kipya na maisha yanakwenda? Kuna sehemu katika maisha mtu ukifika, unajaribu kuacha baadhi ya mambo, ama kutokana na umri au kwa sababu ya nafasi. Kuna mawaziri wengi katika serikali au wabunge ni vijana, ambao wangependa sana kufanya mambo ya umri wao, lakini hadhi yao inawafanya washindwe kujiachia kwa uhuru.

 

Wanakosa uhuru huo siyo kwa sababu wananyimwa, bali nafasi zao hazioni busara wao kufanya hayo yanayofanywa na vijana wenzao.

Wolper Gambe akiwa  na shemela yetu, a.k.a Kibenteni chake, Brown.

Picha na namna hiyo mtu huwezi kushangaa kuona watu kama akina Gigy Money wanazitupia kwa vile tunajua wana ugeni na ustaa na pia ni kama watoto flan hivi wasiojitambua.

 

Lakini sasa mtu kama Wolper, staa wa ukweli wa muda mrefu, mtu ambaye umeshatoka na watu wenye heshima zao na mmoja wa wadada wa mfano hapa Bongo, leo unaenda kutupia picha za namna ile, ni kitu gani hiki? Punguza ushamba bwana! Akaunti yako katika mtandao inatakiwa itumike kwa manufaa yako na watu wanaokuzunguka. Ni vyema kama ungetangaza biashara yako mpya, uombe maoni kwa mashabiki na vitu kama hivyo, sasa kutuonyesha upo chumbani, umejifunika shuka, ndiyo nini sasa?

 

Hivi unafikiri nani hafanyi hayo mambo? Na umeshawaona wangapi wa umri wako wakitupia hayo mapicha kwenye akaunti zao, au unafikiri wao hawapo huko kwenye mitandao? Nakukubali sana katika suala zima la staili ya mavazi yako lakini kwa hili dada yangu sioni sababu ya kukufichia uso. Ifike sehemu uige mfano wa wasanii wengine ambao wanafanya mambo yao ya sanaa kwenye mitandao na kwingineko lakini inapofika wakati wa maisha ya nje ya kazi wanajiheshimu, wanajithamini.

 

Hata kama picha hiyo ilikuwa ni ya kawaida lakini haikupaswa kuonesha uhalisi wa kitandani tena mwanamke na mwanaume, unadhani unatengeneza nini kwenye vichwa vya mashabiki wako. Mbona kiki zingine ni za kujidhalilisha?

 

Mimi nilitegemea kukuona ukija na wazo jipya la kuinyanyua Bongo Muvi kutoka ICU ilipolala. Mambo kama haya ndiyo yanayochangia baadhi ya wazazi kuwakataza watoto wao wanapotamani kuigiza, kwani wanahofia na wao wataingia huku waliko dada zao wakiamini watu wote wa Bongo Muvi wanafanya hivyo. Wolper dada yangu, piga kazi acha huu ushamba, tasnia yenu inahitaji kukombolewa, wewe ni miongoni mwa wanaotegemewa kufanya kitu ili kuinusuru.

BARUA NZITO: GABLIEL NG’OSHA, RISASI JUMAMOSI

Leave A Reply