The House of Favourite Newspapers

Wosia wa Hamad: Baba Yangu Alinitenga, Mali Apewe Mke Wangu – Video

IKIWA ni takribani siku moja tangu kijana aliyekuwa akiishi kwa msaada wa mashine ya kupumulia Awadhi Hamad afariki dunia katika Hospitali ya Mloganzila ambayo ni Tawi la hospitali ya Taifa Muhimbili, juzi Oktoba 17, 2019, mgogoro mkubwa umeibuka baina ya familia yake pamoja na ile ya mke wake.

 

Mgogoro huo unaodaiwa kuwa chanzo chake ni familia ya baba yake Hamad  kumtelekeza kijana wao wakati alipoanza kuugua, ambapo mgogoro huo umesababisha taratibu za mazishi ya kijana huyo kusimama mpaka pale watakapopata muafaka.

 

Akizungumza na Global TV Online msibani nyumbani kwa marehemu Ukonga jijini Dar es Salaam, jana, baba mzazi wa mke wa marehemu, Mzee Beneth Kulekana amesema kuwa, hivi karibuni alikwenda Hospitali kumjulia hali mkwe wake huyo (Marehemu hamad) ambaye alimuomba amwandikie wosia.

 

“Aliniambia, ‘baba, leo nina jambo la kukuambia!, naomba nikiwa nasema uandike wosia wangu, endapo nikifa haya ndiyo yafanyike na si vinginevyo’, nilianza kuandika ambapo alisema baba yake mzazi na ndugu zake walikuwa wamemtenga tangu aanze kuugua.

 

“Alisema akifa, ndugu zake wasirithi mali zake, badala yake mali zake zote zirithiwe na mke wake pamoja na mtoto wake. Iwapo mwili wake utapelekwa kwa baba yake mkubwa, Tabata basi mke wake na mtoto wake wasiende huko kushiriki msiba.

 

“Baada ya kumaliza kuandika nilimsomea, akasema wosia uko sawa, wakati huo hali yake ilikuwa mbaya sana, nikaanza kutafuta mashehe kwa ajili ya kuusaini wosia huo lakini kutokana na hali ya mgonjwa hatukufanikiwa na yeye akawa ametutoka,” amesema Mzee Kulekana.

 

Imeelezwa kuwa, mwili wa Hamad unatolewa Hospitali na kupelekwa moja kwa moja katika makaburi ya Kinyerezi kwa ajili ya maziko hii leo Jumamosi. 

 

Comments are closed.