The House of Favourite Newspapers

Wosia wa Maria, Consolata Waliza Wengi!

KILA nafsi itaonja umauti, tuwaombeeni Maria na Consolata walale mahali pema peponi! Hicho ndicho kinachosemwa na kila aliyewafahamu pacha walioungana mwili, Maria na Consolata Mwakikuti (22) waliofariki dunia usiku ya Jumamosi iliyopita.

 

MAZISHI YA KIHISTORIA

Wakati mazishi yao yakiweka historia leo kwenye Makaburi ya Tosamanga, Iringa kutokana na kuwa msiba wa kitaifa, wosia waliouacha pacha hao umeliza wengi.

DAKTARI ASIMULIA

 

Akielezea wosia waliouacha watoto hao, mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa walikokutwa na umauti pacha hao alisema kuwa, mbali na Consolata kumwambia daktari aliyekuwa anawahudumia kuwa sasa wanakufa, pacha hao walishajua kuwa watakufa muda wowote hivyo kila walipotokewa na hali fulani, waliumia wakijua muda ndiyo umefika na kikubwa walijiandaa kisaikolojia.

“Unajua pacha hawa walipofikisha umri fulani wakati wanaandikishwa shule ya msingi, kuna utaratibu ulitaka kufanyika wa kuwatenganisha, lakini wenyewe walikataa katakata.

HAWAKUTAKA KUTENGANISHWA

“Miongoni mwa mambo ambayo nadhani watakuwa wameyaandika kama wosia na kuacha mahali fulani kwenye makazi yao ni suala hilo la kutotenganishwa hadi wanapelekwa kaburini.

“Hawakutaka kulisikia suala hilo kwa sababu walikuwa wakipendana mno. Kila mmoja hakutaka kutenganishwa na mwenzake hadi umauti ulipowatofautisha kwa dakika kati ya kumi na kumi na tano. “Walisema hata wakifa, wasitenganishwe, wazikwe pamoja, kwenye kaburi moja. Na hilo nadhani litakuwa limezingatiwa kwenye mazishi yao.

 

“Walilisisitiza sana jambo hilo kwamba wazikwe pamoja bila kutenganishwa kutokana na namna walivyopendana,” alisema daktari huyo, jambo ambalo liliungwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Richard Kasesela ambaye aliongeza:

“Miongoni mwa wosia wa Maria na Consolata ni upendo. Mara kadhaa walisisitiza kwamba watu wapendane. “Maria na Consolata walibadilisha kabisa mazingira ya Chuo Kikuu cha Ruaha kutokana na mbegu ya upendo waliyoipanda.

 

“Watu wengi walifika chuoni hapa kwa ajili ya Maria na Consolata na hata siku moja hawakuacha kumuonesha mtu yeyote upendo. “Maria na Consolata wametuachia deni kubwa la kuhakikisha tunadumisha wosia huo wa upendo kama walivyotutaka kufanya.

“Ni jambo hilo ambalo kama unavyoona Mji wa Iringa umezizima, wengi wanalia  kutokana na kumbukumbu za pacha hawa. Walikuwa ni kama nembo ya Mkoa wa Iringa.“Maneno yao juu ya sisi kupendana ndiyo yanaliza wengi.”

TARATIBU ZIMEKAMILIKA

DC Kasesela alimalizia kwa kusema kuwa, shughuli zote mjini Iringa leo zitasimama kwa muda ili kutoa heshima kwa pacha hao na taratibu zote zilikuwa zimekamilika ambapo Maria na Consolata watazikwa kishujaa kwa heshima zote.

 

DAKTARI WA DAR NAYE

Baada ya kutoka Iringa, Risasi Mchanganyiko pia lilizungumza na mmoja wa madaktari waliokuwa wakiwahudumia pacha hao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa taasisi hiyo.

Daktari huyo alisimulia kuwa, kifo cha Maria na Consolata kinasikitisha, hasa ikizingatiwa kuwa Serikali na wadau wengine walitumia gharama kubwa kuokoa maisha yao. Alieleza kwamba, kabla ya kufikishwa Muhimbili na baadaye kupatwa na umauti, pacha hao walitibiwa Iringa na nchini Afrika Kusini, lakini tatizo lao lilishindikana.

 

“Hapa kwetu (Muhimbili) hawakuja kutibiwa, walifikishwa kwa ajili ya support tu. Hospitali hata za nje ya nchi madaktari walishindwa kulishughulikia tatizo lao na kuamua kuwarudisha, lakini kwa sababu ya hali yao kuwa mbaya, ilibidi wafike Muhimbili kwa support,” alisema daktari huyo.

 

SAPOTI YA OKSIJENI

Alipoulizwa walipata support gani walipokuwa hapo Muhimbili, daktari huyo alijibu: “Ile kuwa karibu na madaktari bingwa na kupewa sapoti za kitabibu pamoja na oksijeni.” Kwa mujibu wa daktari huyo, ilikuwa vigumu kuwatenganisha pacha hao kutokana na kuungana sehemu muhimu za miili yao.

HAWAKUPASWA KUZALIWA?

Aliendelea kueleza: “Kitabibu hawakupaswa kuzaliwa. Madaktari wangegundua tatizo hilo wakiwa bado tumboni, ilipaswa madaktari washauri mimba hiyo itolewe, lakini kwa sababu walizaliwa ilikuwa pia haiwezekani kuwatenganisha.”

Kuhusu kutolewa Muhimbili na kurudishwa nyumbani kwa gari la wagonjwa (ambulance), daktari huyo alisema: “Tulifanya hivyo kwa sababu walikuwa bado wagonjwa. Kama nilivyosema ilikuwa hawawezi kupona kutokana na hali yao, hivyo tulichofanya ni kusaidia kusogeza mbele siku zao za kuishi.

“Hapa Muhimbili walipewa mashine ya kupumulia inayojulikana kitaalam kama Oxygen Concentrator , lakini pia walipewa gari la wagonjwa la kuwarudisha nyumbani. Imani yetu ilikuwa mashine hiyo iwasaidie kuongeza siku za kuishi na walielekezwa kwamba wakiona hali inazidi kuwa mbaya, waende hospitali iliyoko karibu kwa msaada wa kitabibu.”

MAISHA YAO KWA KIFUPI KABLA YA UMAUTI

Consolata na Maria walikuwa wameungana kuanzia kiunoni, wanatumia miguu miwili, mikono minne, na vichwa viwili kwa maana kila mmoja na kichwa chake.

Consolata na Maria walizaliwa mwaka 1996 katika Kijiji cha Ikonda Wilaya ya Makete mkoani Njombe. Walipata elimu yao ya msingi kijijini hapo na kufanikiwa kufaulu vizuri kabla ya mwaka 2011 kuchukuliwa na wamisionari na kupelekwa wilayani Kilolo kwa ajili ya kuwalea zaidi katika Kituo cha Nyota ya Asubuhi Kidabaga wilayani Kilolo. Walianza kujulikana wakiwa shule ya msingi.

Wakiwa na umri wa miaka mitatu, baba yao, Alfred Mwakikuti alifariki dunia na walipofika darasa la pili mwaka 2002, mama yao pia alifariki dunia hivyo kuwaacha yatima. Katika maisha yao ya kusoma, kila mmoja alikuwa na madaftari yake na wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika. Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi! Amina!

STORI: Mwandishi Wetu, Iringa na Dar

Comments are closed.