The House of Favourite Newspapers

YA ROMA , ULIMBOKA YAJIRUDIA KWA MO

Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’

YALIYOJIRI baada ya kutekwa, kuteswa na kureshwa uraiani kwa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’ na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven Ulimboka yanadaiwa kujirudia kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’, Ijumaa limedokezwa.  MO alitekwa na watu wasiojulikana Oktoba 11, mwaka huu alipokuwa akiingia kwenye Hoteli ya Colessium, Oysterbay jijini Dar kwa ajili ya mazoezi binafsi.

Kutoka kwa vyanzo vyake vya kuaminika, Ijumaa lilitonywa kuwa, watu wote waliotekwa, mara tu baada ya kurejea uraiani iliaminika wangesimulia walichokutananacho, lakini hakuna aliyewahi kuthubutu kufungua kinywa kueleza kilichompata. Ilielezwa kwamba, hicho ndicho kinachojitokeza kwa MO ambaye mbali na kumshukuru Mungu, Rais na Watanzania kwa kumuombea, hajaeleza hasa ni nini kilichompata au alichokumbana nacho huko alikokuwa baada ya kutekwa.

DK ULIMBOKA

Juni, 2012, watu wasiojulikana walimteka Dk Ulimboka na kumpeleka kwenye Msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar ambako huko aliteswa hadi akapoteza fahamu. Ilifahamika kwamba, Dk Ulimboka alipigiwa simu na watu ambao walimteka na kumpeleka huko Mabwepande ambako aliokotwa na wasamaria wema akiwa hajitambui.

Dk Ulimboka alitekwa usiku wa saa 6:00 na watu watatu waliokuwa na silaha aina ya short gun na bastola; tukio lililojiri kwenye Barabara ya Tunisia, Kinondoni jijini Dar. Baada ya kutokea tukio hilo, Watanzania wengi walitamani kumsikia Dk Ulimboka akieleza ni nini hasa kilimpata, lakini mpaka leo, yapata miaka sita, hajawahi kufungua kinywa kusimulia mkasa huo na wala hasikiki.

ROMA MKATOLIKI

Ilikuwa Aprili, 2017 ambapo Roma na wasanii wenzake, Moni Central Zone, Bin Laden na Imma ambaye alikuwa mfanyakazi wa Studio za Tongwe Records zilizopo Masaki, Dar, walitekwa na watu wasiojulikana walipovamiwa wakiwa studio.

Utekwaji huo ambao ulitikisa nchi ulifanyika majira ya saa 1:30 usiku. Hata hivyo, haikujulikana sababu za utekaji wa Roma na wenzake hivyo walipopatikana baada ya kutupwa huko Ununio jijini Dar, Watanzania walitamani kujua kilichowapata. Roma na wenzake waliahidi kuzungumza kila kitu, lakini hadi leo ukiwauliza hakuna aliye tayari kueleza walichokumbana nacho.Image result for mo dewji

MO

Kama ilivyokuwa kwa Roma na Dk Ulimboka, mara baada ya kurejeshwa na kutupwa kwenye Viwanja vya Gymkhana, Dar, MO hakuwa tayari kueleza alikokuwa na nini kilichompata. Hata hivyo, baada ya kuona siku zinayoyoma bila kueleza kilichompata, waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliendelea kumsaka ili azungumze na ndipo baba yake, Gulam Hussein Dewji akaomba mwanaye aachwe apumzike.

“Mohammed hajambo, anaendelea vizuri. Ninachoweza kusema kwa sasa mwacheni mwanangu apumzike,” alisema baba mzazi wa MO. Bado sakata la MO lipo mikononi mwa uchunguzi wa kipolisi ambapo watu kadhaa wanashikiliwa kusubiri uchunguzi ukamilike ili kufikishwa mahakamani

Stori: Sifael Paul, Ijumaa

Comments are closed.