The House of Favourite Newspapers

Ya Zanzibar; ni Jecha au mawazo ya wakubwa?

0

YANAYOENDELEA visiwani Zanzibar kuhusu kufutwa na kutangazwa upya kwa tarehe ya uchaguzi mkuu yanafahamika. Nyongeza ya tafakuri yangu ni: Kwa nini kama taifa tunalazimika kulipigia mstari jibu ambalo hatuna uhakika nalo?

Tangu watawala hadi watawaliwa kwa pamoja wanakubaliana na hali tete ya amani katika visiwa hivyo, kilichosalia ni kujiuliza nini kifanyike kujenga palipo bomoka?

Jecha Salum Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) anayebeba msalaba wa lawama za kuvuruga uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, ameibuka na wazo la kurudia uchaguzi akiwa tayari amepanga na tarehe ya kufanyika kwa zoezi hilo.

Kinachonishangaza ni wazo lake kukubaliwa mapema mno na wakubwa wa nchi ambao wanatoka chama tawala cha CCM! Hoja za kuwa Jecha alitumwa na chama hicho tawala kuvuruga uchaguzi kwa kile kinachotajwa kuwa ni dalili za watawala kushindwa hazijajibiwa.

Sura mbele ya kioo cha fikra inaonesha kuwa huenda wakubwa wa Zanzibar au wa muungano walijitekenya na ‘figisufigisu za uchaguzi uliovurugika’ na sasa wanacheka wenyewe licha ya ukweli kwamba akili ya Jecha haiwezi kuondoa tatizo lililoanzishwa na akili yake ileile.

Nastaajabu; kwa nini kauli za Jecha zimekuwa ni za mwisho katika sakata la uchaguzi Zanzibar? Je, ni mawazo yake au anatumwa na wakubwa ndiyo maana hahojiwi kila anapofanya tukio lenye maswali mengi?

Ni kiwango gani cha elimu kinahitaji kujua kama mkuu huyo wa Zec alikiuka kifungu cha 119 cha sheria ya uchaguzi Zanzibar namba 11 ya mwaka 1994 inayoagiza maamuzi ya tume lazima yapate uhalali na theluthi 2 ya wajumbe wote?

Jecha alipofuta matokeo inaelezwa kuwa hakupata baraka za wajumbe wenzake. Alichotoka nacho nje ya ukumbi kuliambia taifa ni kwamba tume yake imeingiwa na ‘mdudu’ wa kutoelewana kwa wajumbe hadi kufikia hatua ya kuchapana makonde lakini hakuwataja waliotiana judo ndani ya Zec.

Hakuishia kukwama kuthibitisha hilo, alisema pia kwamba kuna baadhi ya maeneo hasa Pemba idadi ya wapiga kura ilikuwa imezidi, hiki nacho kilikuwa kioja kingine kwa sababu Jecha hakuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa vyama shiriki juu ya kasoro hiyo.

Hii ina maana kwamba uamuzi wake wa kufuta matokeo una ukakasi mwingi; lakini cha ajabu amekuja na ngonjera mpya ya kurudia uchaguzi kupitia tume yake ileile. Bila aibu amefanya hivyo bila kuwa na majibu ya kuzaliwa upya kwa tume yake.

Angelikuwa muungwana angesema anarejea uchaguzi kwa sababu ameitakasa tume yake; wajumbe waliotwangana makonde amewapatanisha, wingi wa idadi ya waliojiandikisha Pemba umepatiwa ufumbuzi na kwamba tume yake imetakasika vya kutosha.

Kama nilivyosema kwa nini kama taifa tunapigia mstari jibu tusilokuwa na uhakika nalo? Tunapomkubalia Jecha arejee uchaguzi wakati chama kikuu cha upinzani, Cuf kinagomea tunatarajia nini? Hatuoni Jecha anatukimbiza kwenye mvua na kutuingiza baharini?

Kwa uamuzi huu, hatuoni kama tunairejesha Zanzibar enzi za uhasama na utengano uliokuwa ukitekelezwa na chama cha Zanzibar Nationalist (ZNP) kilichotetea usultani na kile cha Afro-Shiraz (ASP) kilichopigania watu weusi?

Je, tunataka kukubaliana na msemo wa jasiri haachi asili na kwamba tumekubali Jecha aitoe Zanzibar kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuipeleka kwenye vuguvugu jipya la ubaguzi lililozikwa mwaka 1964 baada ya kufanyika mapinduzi?

Naamini tulikuwa na njia nyingine ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar siyo hii ya kurudia uchaguzi kwa sababu zoezi hili haliwezi kufuta hisia za Wazanzibari kwamba hawa wanaonewa na wale wanapendelewa kama ilivyokuwa enzi za ASP na ZNP.

Leave A Reply