Yah TMK Waipiga Mkwara Jahazi

Kundi la Muziki wa Taarab Yah TMK

KUNDI la Muziki wa Taarab linakuja kasi katika anga la burudani, Yah TMK wamechimba mkwara wa maana kwa wapinzani wao Jahazi Modern kuelekea mchuano mkali wa Nani Mkali Wako utakaofanyika Aprili Mosi,mwaka huu ambayo ni Sikukuu ya Pasaka kwenye Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem, Dar.

 

 Yah TMK wametoa mkwara huo kupitia mwimbaji na kiongozi wao mahiri kabisa,Omarry Tego ambaye ataongoza mashambulizi makali kwa upande wa timu yake iliojaza waimbaji machachari.Akizungumza na Mikito Nusu Nusu, Tego alisema kuwa wamejipanga kuwagaraza wapinzani wao kwa kuwa pambano hilo litakuwa likifanyika kwenye uwanja wao wa nyumbani.

 

“Kwanza kabisa kwetu kila kitu kipo sawa lakini kwa upande mwingine,Dar Live ni kiwanja chetu cha nyumbani kwa kuwa tunapiga shoo kila siku ya Jumatano, naamini hawatoweza kutoka siku hiyo kutokana na maandalizi yetu yalivyokuwa makubwa.

“Unajua kwa kipindi kirefu sisi tulikuwa tunawasaka  waingie kwenye anga zetu na kwa kuwa wamejileta lazima tutawaonyesha kwa sisi ni akina nani siyo kikubwa tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kushuhudia tunavyoliamsha dude,”alisema Tego.

 

Kwa upande wa mratibu wa shoo hiyo naMeneja wa Dar Live, Rajab Mteta ‘KP Mjomba’ alisema mbali ya mchuano huo kutakuwa na vita nyingine ya wakali wa Muziki wa Singeli nchini itakayokwenda kwa jina la Mwisho wa Ubisi ambapo vichwa vikali vitachuana vikiongozwa na Man Fongo, Sholo Mwamba na Dullah Makabila.

 

KP Mjomba aliongeza kuwa kiingilio katika shoo hiyo ya aina yake kitakuwa ni buku saba yaani shilingi 7,000 huku michezo mbalimbali ya watoto ikiwemo kama vile kuogelea itafanyika kuanzia saa nne asubuhi hadi 12 jioni kwa mtonyo wa buku tatu yaani shilingi 3000.

Na Mikito Nusu Nusu.
Toa comment