The House of Favourite Newspapers

Yajue magonjwa mapya manne ya zinaa yanayowachanganya wataalam

 

MAGONJWA mapya huibuka kila uchao, na magonjwa yaambukizwayo kwa ngono ni miongoni mwao.

 

Hawa ni bakteria wanne ambao husababisha magonjwa makali ya zinaa ambayo yanaweza kuleta tishio la afya ya jamii.

 

1 Neisseria meningitides

 

Neisseria meningitidis, pia hufahamika kama meningococcus,  husababisha uvimbe hatari wa tando za uti wa mgongo na ubongo. Lakini, bakteria huyo sasa anapata umaarufu zaidi kwa kusababisha maambukizi kwenye maungo ya uzazi.

 

Utafiti uliofanywa miaka ya 1970 ulibainisha ni kwa namna gani dume moja la sokwe alihamisha bakteria hao hatari kutoka mdomoni na puani kwenda kwenye uume wake baada ya kujilamba sehemu zake nyeti.

 

“Mnyama huyu (sokwe) mara kwa mara hujilamba uume wake,” waandishi wa utafiti huo walibaini.

 

Takribani asilimia 10 ya watu wazima wana bakteria aina ya Neisseria katika makoo na pua zao. Tafiti zinabainisha kuwa wanaweza kuhamisha bakteria hao kupitia mabusu makali yahusishayo ndimi, ama kunyonya sehemu za siri za watu ambao hawana bakteria hao.

 

Watafiti hata hivyo hawana hakika ni kwa nini bakteria hao wamesambaa kwa kasi na kuzua ugonjwa hatari kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja barani Ulaya, nchini Marekani na Canada.

 

Hata hivyo, utafiti mmoja juu ya uwasho mkali wa mrija wa kupitisha mkojo toka kweye kibofu unaosababishwa na bakteria huyo ulibainisha kuwa wanaume walipata maambukizi hayo kupitia ngono ihusishayo mdomo.

 

Wanasayansi wanaamini kuwa, maambukizi makali ya bakteria huyo yaliyokumba kwa nguvu miji kadhaa ya Marekani mwaka 2015 yalichochewa na vinasaba vya karibu vya bakteria wa familia moja ya Neisseria gonorrhoeae, ambaye husababisha ugonjwa mwengine wa zinaa wa kisonono.

 

Ukaribu wa bakteria hawa ulisababisha kusambaa kwa haraka kwa maambukizi hayo hatari.  Kuna aina tano ya bakteria hatari wa Neisseria meningitidis duniani, lakini kwa bahati nzuri kuna chanjo za aina mbili ambazo zinapatikana na zinakinga dhidi ya aina zote za bakteria hao.

 

2. Mycoplasma genitalium

Mycoplasma genitalium, moja ya bakteria wadogo zaidi wanaofahamika, wanapata umaarufu mkubwa zaidi ya maumbo yao kwa kusabisha maambukizi hatari ya ugonjwa wa zinaa.

 

Bakteria huyo aligunduliwa miaka ya 1980, na leo hii anaambukiza asilimia moja mpaka mbili ya watu hususani vijana.

 

Maambukizi ya Mycoplasma genitalium ambayo kwa kawaida hayana dalili, wakati mwengine hufanana na dalili za kisonono na kaswende kwa kuwashwa mfululizo kwa mrija wa mkojo kwa wanaume na mlango wa kizazi kwa wanawake.

 

Kutokana na  kusababisha maumivu makali ya nyonga kwa wanawake, bakteria huyo anahusishwa pia na ugumba, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa watoto njiti na hata kufariki watoto tumboni kwa mama.

 

Japokuwa kondomu inaweza kuzuia maambukizi yake, watafiti wanatoa tahadhari juu ya usugu wa bakteria huyo kutibika na dawa za antibaiotiki za azithromycin na doxycycline.

 

3. Shigella flexneri

Shigellosis husababishwa kwa kugusa moja kwa moja au kwa njia moja au nyengine kinyesi cha binadamu. Maambukizi ya bakteria ho husababisha maumivu makali ya tumbo, na kuhara damu ambapo hustawisha kusambaa kwa bakteria hao.

 

Ijapokuwa ugonjwa huo umekuwa ukionekana zaidi kwa watoto na wasafiri kwenye nchi zenye uchumi mdogo na wa kati, watafiti walianza kupokea matukio ya ugonjwa huo kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja toka miaka ya 1970.

 

Ugonjwa huo, wanasayansi wanaamini, umechukuwa njia mpya ya maambukizi kwa kutumia ngono ya  kinyume na maumbile,  na ngono inayohusisha midomo na kusabisha maambukizi kadhaa ya gonjwa hilo la zinaa kwa miongo minne sasa

 

4. Lymphogranuloma venereum (LGV)

LGV mwanzo hutokea kama kipele ama lengelenge na kisha hushambulia mfumo wa kinga ya mwili na hivyo kusababisha uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi. Ugonjwa huu pia husababisha maambukizi katika njia ya haja kubwa na pia husababisha maumivu makali ya tumbo.

 

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.