LEO tutazungumzia magonjwa ambayo yana chanjo kwa watoto kama vile chanjo za surua, kichaa cha mbwa, dondakoo, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na nimonia. Tuanze kuchambua ugonjwa mmojammoja:
SURUA
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenea kwa haraka. Ugonjwa huathiri watu wa rika zote, lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi.
Ugonjwa wa surua huenezwa kwa njia ya hewa hasa pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya na maambukizo huwa ni ya haraka sana hasa sehemu zenye msongamano. Ugonjwa wa surua kwa watoto huzuilika kwa chanjo ya surua. Mtoto hupata sindano mbili za kumkinga na surua ambayo hutolewa kwenye bega la kushoto akamilishapo umri wa miezi tisa na marudio baada ya mtoto kutimiza miezi 18.
KICHAA CHA MBWA
Ni ugonjwa unaowapata paka au mbwa endapo mnyama wa porini mwenye ugonjwa atamuuma mbwa au paka ambaye hajapata chanjo.
Watoto na hata watu wazima wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa baada ya kuumwa na mbwa au mnyama wa porini mwenye ugonjwa huo. Mzazi au mlezi hakikisha chanjo ya kuzuia ugonjwa wa kichaa cha mbwa na wanyama wa nyumbani kama vile mbwa na paka wanapata kila baada ya miezi 6 ili wasipatwe na maradhi haya.
DONDAKOO
Ni ugonjwa unasababishwa na vimelea vinavyoshambulia sehemu za koo na huenezwa kwa njia ya hewa, mate au majimaji yanayotoka kwenye sehemu za maambukizo. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na kuwa na vidonda kooni, kutoa kamasi iliyochanganyika na damu na kuwa na maumivu wakati wa kumeza chakula. Ugonjwa huu unawapata watoto wadogo. Hakikisha mtoto anapata dozi tatu za chanjo ya kuzuia dondakoo ili kumpa kinga kamili.
HOMA YA INI
Ni ugonjwa hatari unaosababishwa na maambukizi ya virusi viitwavyo Hepatitis B. Ugonjwa huu unaweza kuwapata watu wa rika zote lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi. Ugonjwa huu ni hatari na huambukizwa kwa haraka zaidi hata Ukimwi. Njia za maambukizi ni sawa na zile zinazoambukiza VVU, mfano kuongezewa damu yenye virusi, kutumia vifaa visivyotakaswa kama vile mabomba ya sindano, nyembe na kadhalika; kutoka kwa mama mwenye virusi kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua au kunyonyesha; kujamiana na mtu mwenye maambukizo bila kutumia kinga nk.
Ugonjwa wa homa ya ini hauna tiba na ni hatari zaidi ya Ukimwi. Hakikisha mtoto anapelekwa kituo cha huduma ya afya apate utaratibu ili apate dozi kamili ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa homa ya ini.
UTI WA MGONGO, KICHOMI
Husababishwa na vimelea aina mbalimbali na huathiri zaidi watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Magonjwa haya huambukizwa kwa njia ya matone ya mate yenye uambukizo kutoka kwa mtoto anayekohoa au kupiga chafya.
Vilevile huenea kwa kubadilishana vitu vya kuchezea kama vile midoli na vitu vingine vilivyowekwa mdomoni. Muda wa maambukizo mpaka ugonjwa ujitokeze ni siku 2 – 4, hapo ndipo dalili za awali hutokea. Magonjwa haya ni hatari kwani huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha madhara kama kutosikia vizuri, upofu, mtindio wa ubongo na hata kusababisha kifo cha mtoto. Hakikisha mtoto anapata chanjo ya kuzuia magonjwa haya.
NIMONIA
Huenea kwa njia ya hewa wakati mtu mwenye vimelea anapopiga chafya au kukohoa. Ugonjwa huu pia unaweza kuambukizwa kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea vya maradhi haya kama nguo, leso, vikombe, vitu vya kuchezea watoto nk. Mpeleke mtoto akapate chanjo ya nimonia akamilishapo umri wa wiki sita.
Comments are closed.