The House of Favourite Newspapers

YAJUE YANAYOSABABISHA UGUMBA KWA WANAWAKE !

MOJA ya sababu kubwa inayomfanya mwanamke kuwa mgumba ni ile ya mirija ya uzazi ya mwanamke kuvimba kwa kujaa majimaji na kuziba upande wa mwishoni mwa mirija. Hali hiyo ni hatari na kitaalamu huitwa Hydrosalpinx. 

 

Mirija hii inapovimba huwa na uvimbe mkubwa, uvimbaji huu na kuziba huwa wa pande zote mbili, kulia na kushoto. Tatizo hili la kuvimba na kuziba kwa mirija husababisha ugumba kwa mwanamke. Pamoja na kujaa maji pia mirija inaweza kujaa usaha au kujaa damu. Tatizo hili huweza kumfanya mwanamke apoteze uwezo wa kuzaa yaani kuwa mgumba.

 

Chanzo kikuu cha hali hii ni maambukizi katika viungo vya uzazi, ‘Pelvic Inflammatory Disease’ au kwa kifupi ni ‘PID’. Maambukizi haya hupanda taratibu na huanzia ukeni. Kwa hiyo mwanamke anayesumbuliwa na tatizo la maambukizi ya mara kwa mara ukeni ni vema atibiwe vinginevyo baadaye anaweza kujikuta anashindwa kupata ujauzito.

 

Dalili za maambukizi ya mara kwa mara ukeni ambayo yanaweza kukufanya ukose uwezo wa kuzaa kwa kupata tatizo hili ni kutokwa na uchafu au majimaji ukeni yenye harufu mbaya na muwasho, maumivu ukeni, maumivu wakati wa kujamiiana na kuhisi uvimbe ukeni kama gololi. Ingawa siyo kila maambukizi ya kizazi husababisha kuziba mirija, bali endapo mwanamke atawahi hospitali na kupata tiba sahihi anaweza kupona na asiwe mgumba.

 

Mwanamke mwenye tatizo hili hutokea mirija inapoharibika maana yake yai haliwezi kuchukuliwa na kuingizwa katika mirija ya mbegu za kiume kwani haliwezi kupenya. Matatizo mengine yanayosababisha mirija ya uzazi ya mwanamke kuziba ni makovu kutokana na upasuaji wa awali wa kizazi au mirija, tabaka la ndani la kizazi kuwa nje ya kizazi na saratani ya mirija ya uzazi au vifuko vya mayai.

DALILI KWA MGONJWA

Kwa ujumla dalili hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke lakini zipo dalili kuu za ugonjwa. Dalili kuu ni mgonjwa mwenye tatizo hili kulalamika maumivu ya mara kwa mara ya tumbo chini ya kitovu na husambaa katika nyonga zote na kiuno. Wapo wagonjwa wengine hawaoneshi dalili zozote ila wakipimwa kwenye ‘Ultrasoud’ au ‘HSG’ huambiwa mirija imevimba au imejaa usaha.

 

Dalili nyingine ni mwanamke kulalamika kutoshika mimba kwa zaidi ya mwaka tangu aanze kuitafuta, tumbo kuuma mara kwa mara hasa anapokuwa katika siku zake za hedhi. Lakini pia mzunguko wa hedhi huvurugika na kutoona ute wa uzazi, kupoteza hamu na raha ya tendo la ndoa, ingawa mwanaume akipimwa mbegu za uzazi huwa vizuri.

 

TIBA

Mgonjwa lazima akafanyiwe uchunguzi katika kituo cha afya na madaktari wa magonjwa ya akina mama katika hospitali na daktari akigundua tatizo atakupa dawa stahiki.

Comments are closed.