The House of Favourite Newspapers

Yale ya Fakhi, Yanga Yampiga stop Cannavaro

0
Beki wake wa kati wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Ibrahim Mussa | Championi Ijumaa | Habari

BAADA ya kuvuliwa ubingwa wa Kombe la FA na Mbao FC, uongozi wa Yanga umeliondoa jina la beki wake wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.

Cannavaro ataukosa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, sambamba na beki Mtogo, Vincent Bossou na mshambuliaji Mzambia, Donald Ngoma kutokana na kuandamwa na majeraha.

Yanga inayotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kwa sasa inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56, nyuma ya vinara Simba wanaoongoza wakiwa na pointi 59. Simba imebakiwa na michezo mitatu huku Yanga wakiwa nayo mitano.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, amelithibitishia Championi Ijumaa kuwa, beki huyo hatakuwepo katika mchezo wa kesho kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu alizopata katika michezo yao iliyopita.

“Wachezaji ambao watakosa mchezo wa Prisons nje ya majeruhi ni Cannavaro peke yake kwa sababu ya kutumikia adhabu ya kuwa na kadi tatu za njano ambazo alizipata katika mechi zilizopita lakini kwa wachezaji wengine kila kitu kipo sawa,” alisema Saleh.

Beki Mohammed Fakhi.

Championi lilimtafuta beki huyo ambaye alisema: “Kiukweli najisikia vibaya kuukosa mchezo wa Jumamosi dhidi ya Prisons kwa kuwa nina kadi tatu za njano lakini wenzangu watakaokuwepo, naamini watafanya kazi
kubwa ya kutimiza majukumu yao ili tutetee ubingwa wetu.

” Ishu ya kadi tatu za njano, ndiyo ambayo imesababisha kizaazaa katika soka la Tanzania, kufuatia Simba kuikatia rufaa Kagera Sugar kudai pointi tatu za mezani kutokana na kumchezesha beki Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.

Awali, Kamati ya Saa 72 iliipa Simba pointi tatu za bure lakini Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ikazirejesha pointi hizo kwa Kagera. Katika mchezo wa uwanjani, Kagera ilishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Simba imejipanga kwenda kushtaki kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Leave A Reply