The House of Favourite Newspapers

YAMEMKUTA! Kilichompata Njemba Huyu, Hatasahau

DAR ES SALAAM: Yamemkuta! Ndivyo unavyoweza kusema. Kijana aliyefahamika kwa jina moja la Rama, Jumatatu iliyopita alijikuta akilamba kibano ‘hevi’ kutoka kwa maafande wa jeshi la polisi wakati alipokuwa akitaka kuwapiga chenga ya mwili wanausalama hao; eti awatoroke.

 

Tukio hilo lililotokea kama vile sinema, lilinaswa live na kachero wetu ambaye alifotoa picha kadhaa wakati mtuhumiwa akitolewa chumba cha mahabusu ya Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar kupelekwa kizimbani kusikiliza shtaka lake.

 

Kijana huyo akiwa na kundi la wenzake sita, wote walikuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi ambayo ndiyo ilikuwa imefika mara ya kwanza mahakamani hapo. Baada ya kufunguliwa geti la mahabusu na kuanza kuongozwa na askari polisi kijana huyo alijifanya mjanja kwa kujaribu kujichanganya na watu na kutaka kukimbia.

 

“Unajua jamaa anaonekana alishasoma jinsi mahakamani hapa palivyo, hivyo akajua kuna mwanya wa kuweza kuchomoka endapo askari anayewalinda hatakuwa makini. “We’si umeona, jamaa aliangalia huku na huku, akawaona watu mbalimbali wanaokuja mahakamani na kwa vile alikuwa amevalia vizuri (shati, jinzi na sendozi), akaona ni rahisi kujichanganya nao kisha kutoka nduki,” alisikika shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ally Kitou.

 

Kitendo hicho kilizua taharuki na vurugu mechi mahakamani hapo ambapo polisi walianza kumkimbiza baada ya kuishtukia janja yake. Fasta sana, mmoja wa polisi aliyekuwa akiwasindikiza washtakiwa hao, aliongoza mapambano kwa kula naye sahani moja na kufanikiwa ‘kumtaiti’ kabla hajafika mbali.

Kitendo hicho kilionekana ‘kumkosti’ kijana huyo ambaye alipewa kibano hevi kisha kukunjwa kwa staili iliyopatizwa jina na vijana wa kileo ya ‘Kamata Ticha Ayubu’.

 

“Duh ile staili waliyomtaiti yule jamaa ni balaa maana pale huwezi kufurukuta kwa chochote, kinachobaki ni kutii sheria tu,” alisema shuhuda wa tukio. Polisi huyo kwa ustadi mkubwa na mbinu za kijeshi, alionekana ‘kumbinya’ maeneo maalum jamaa huyo ambaye alionekana tu kuugulia maumivu.

 

“Mwenyewe kaufyata. Unajua vitu vingine ni vya kujitakia, wewe unamuona askari ana silaha kama vile, unajifanya kumtoka kiboya namna ile unategemea nini? Pale angeweza hata kupigwa risasi ya mguu kama polisi angeona anazidiwa spidi,” alisikika shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John Mateo.

 

Baada ya kutaitiwa, mtuhumiwa huyo alipelekwa chumba cha mashitaka na kupandishwa kizimbani mbele ya hakimu Boniface Lihamwike ambaye alimsomea shitaka lake ambapo alikana shitaka hilo. Baada ya kukana shitaka hilo Hakimu Lihamwike alimwambia dhamana yake iko wazi lakini mpaka mwandishi wetu anaondoka mahakamani hapo hakukuwa na jamaa yeyote wa kumuwekea dhamana aliyejitokeza.

 Stori: Richard Bukos, Amani.

Comments are closed.