The House of Favourite Newspapers

Yanayosababisha Kutokuwa Sawa Katika Tendo la Ndoa

0

WIKI hii mpenzi msomaji wangu tutaangalia jinsi tatizo hili la kutokuwa sawa katika tendo la ndoa linavyotokea. Tatizo hili tunaliweka katika makundi manne. Kwanza ni kutokuwa na hamu na hisia ya tendo la ndoa au kitaalamu tunaita Sexual Desire Disorder.

 

Hapa hamu na hisia zinaweza zisiwepo kabisa, yaani usiwe kabisa na hamu au hisia ya tendo. Hii ni hali ya jumla lakini, wengine hutokewa na hali ya kupoteza hamu na hisia kwa mpenzi aliye naye tu ila akienda kwa mwingine hufurahia, hali hii inaweza kutokea kwa mwanaume au mwanamke.

 

Mtu pamoja na kuwa katika hali hii, lakini inaweza kutokea mtu akawa na hamu kidogo sana au ikawa inatokea kwa vipindi fulanifulani baadaye ikapotea. Hii inatokana na upungufu wa vichocheo vya Estrogen kwa wanawake tu na Testosterone kwa wote wanaume na wanawake.

 

Vyanzo vingine katika hili ni umri mkubwa hasa kwa wazee, uchovu wa mwili kutokana na kazi au ulevi, hali ya ujauzito, matumizi ya baadhi ya madawa na magonjwa ya akili. Pili ni kutokuwa na msisimko wa tendo la ndoa hali iitwayo kitaalamu Sexual Arousal Disorders.

 

Hali hii kwa mwanamke huitwa ubaridi wa hisia za mwili na kwa mwanaume huitwa ukhanithi ambapo kwa sasa mwanaume mwenye hali hii ya kutokuwa na msisimko ni yule ambaye uume wake hausimami kabisa kwa kuwa hana msisimko wa mapenzi.

 

Kutokuwa na hisia na msisimko, maumivu wakati wa tendo husababisha usifike kilele cha tendo la ndoa. Kutokuwepo msisimko wa kutosha katika uume na ukeni kutokuwa na majimaji
ya kulainisha uke huwa ni tatizo linalotokana na magonjwa katika viungo vya uzazi na vichocheo. Magonjwa sugu kama kisukari, moyo, kansa, ini, figo huchangia hali hii ya kupoteza msisimko.

 

Tatu ni uume kutokuwa na nguvu au Erectile Dysfunction. Uume ukikosa nguvu maana yake huwezi kufanya tendo la ndoa. Hali hii husababishwa na magonjwa ya mishipa ya fahamu ya uume na mengine yote sugu ambapo tumeyaelezea ambayo huathiri msukumo wa damu katika uume. Uume kukosa nguvu husababishwa na tatizo la kisaikolojia au la mwili kwa ujumla.

 

Nne ni tatizo la kuwahi kumaliza tendo la ndoa kitaalamu tunaita Premature Ejaculation. Tunaposema kuwahi kumaliza tendo la ndoa ni pale mwanaume anatoa manii kabla ya mwanamke unayeshirika naye hajafikia kileleni, ingawa hakuna muda maalumu wa kumaliza tendo la ndoa, ila inatakiwa mwanaume asimalize tendo la ndoa yaani usitoe manii chini ya dakika mbili. Endapo utamaliza tendo chini ya dakika hizo mbili basi tunasema una tatizo hili la Premature Ejaculation.

 

Tatizo hili linaweza kuwa sugu kwako kama hutazingatia ushauri wa kujitibu kwa njia mbili za kujizuia kuwahi, muone daktari wa masuala ya uzazi akusaidie jinsi ya kuwa imara na usiwahi ingawa mazoezi ya kegel ndiyo tiba kubwa. Pamoja na matatizo haya makuu manne, yapo pia mengine ambayo huathiri kwa kiasi kikubwa matatizo haya kama vile kutofika kileleni ambapo mtu anapata msisimko kama kawaida anafanya tendo vizuri lakini hafiki kileleni. Lingine ni maumivu wakati wa tendo.

 

Mwanaume anaumia uume na mwanamke anaumia ukeni, vilevile wengine huugua baada ya tendo hasa pale wanapofikia kileleni mfano mwili wote kuuma na kuchoka, kuumwa kichwa. Matatizo haya tunakuja kuyazungumzia kwa undani katika mada yake.

 

NINI CHA KUFANYA?

Endapo unahisi una matatizo kama haya, basi muone daktari wa masuala ya uzazi katika hospitali ya mkoa. Mengine tayari tulishayazungumzia katika makala zilizopita juu ya utatuzi wake kwa hiyo unaweza pia kupitia katika tovuti ya Global Publishers makala za afya.

Leave A Reply